Ukraine: Baina ya ndoto na jinamizi
2 Desemba 2013Wakati huo katika majira ya baridi mwaka 2004 watu walijitokeza mitaani wakidai demokrasi zaidi na hali bora ya baadaye ya nchi yao. Hivi sasa wanaandamana tena.
Kwa mara nyingine tena suala la demokrasi na hali ya baadaye ya nchi yao ndio linalowasukuma kuingia mitaani. Na kwa mara nyingine tena kuna mtu anyehusika na hali hiyo. Viktor Yanukovich. Kwa mara nyingine tena suala ni iwapo demokrasia nchini Ukraine iendelee ama nchi hiyo ibakie katika udikteta.
Waandamanaji waliingia mitaani wakati huo dhidi ya Viktor Yanukovich, kwa kuwa alitaka kuwa rais, lakini kabla ya uchaguzi kulikuwa na udanganyifu. Kwa hivi sasa ndie rais wa Ukraine.
Rais haaminiki tena
Lakini watu wanaandamana dhidi yake, kwa kuwa hawamuamini tena, kwamba ataielekeza nchi hiyo kuelekea mataifa ya Umoja wa Ulaya. Na wanaandamana dhidi yake , kwa kuwa wanashaka , kwamba anataka kuwanyang'anya sio tu mtazamo wao kuelekea Ulaya lakini pia demokrasia yao.
Zaidi ya watu laki moja waliingia mitaani siku ya Jumapili katika mji mkuu wa Ukraine Kiev wakipinga serikali na pia dhidi ya rais. Wamejitokeza kutoka kila sekta ya nchi hiyo. Wanafunzi, wafanyakazi, lakini pia watu wazima, pamoja na familia zikiwa na watoto licha ya wasi wasi wao kuwa maandamano hayo yanaweza kugeuka ya ghasia.
Ni mbinyo ambao hautakoma dhidi ya serikali na rais kutokana na kushindwa kutia saini makubaliano na Umoja wa Ulaya na ghafla bila kutarajia kutangaza kuwa atashirikiana kwa karibu na Urusi.
Kwa muda wa siku kadha sasa wananchi wanaandamana dhidi ya uamuzi huo. Kwasababu wanaona ndoto yao ikiporomoka, ndoto ya kukaribiana na mataifa ya Umoja wa Ulaya , ya demokrasia na hali bora baada ya kuona hali ilivyo katika mataifa ya Umoja huo, na hivi sasa huenda ndoto hiyo ikawa jinamizi. Hii ni kutokana na mbinyo wa nchi jirani ya Urusi na Belarus.
Matumizi ya nguvu
Hii ilitoa sura ya kutisha mjini Kiev usiku wa Jumamosi, wakati kikosi maalum cha jeshi kilipochukua hatua za kuwakabili kwa matumizi ya nguvu waandamanaji na bila kutoa tahadhari dhidi ya maandamano ya amani yanayounga mkono nchi hiyo kukaribiana na mataifa ya Ulaya.
Upinzani , ambao umekuwa kwa miaka kadha ukipambana kutaka kubadilisha hali ya kisiasa nchini humo unapata uungwaji mkono katika maandamano hayo. Maandamano zaidi yataendelea. Lakini kwa sasa haifahamiki vipi uongozi wa Ukraine utalishughulikia suala hilo.
Mwandishi : Bernd Johann / ZR / Sekione Kitojo
Mhariri: Gakuba Daniel