Ukosefu wa kazi wapungua Ujerumani
2 Mei 2007
Ukosefu wa kazi nchini Ujerumani unazidi kupungua na kwa mara ya kwanza tangu miaka 4.5 mwezi uliopita wa April,umeteremka chini ya milioni 4:
Hivi sasa ni watu milioni 3.967 hawana kazi.Hii ni kasori watu 141.000 ukilinganisha na ilivyokua Machi,2006.Na ni watu 824,000 kasoro kuliko ilivyokua mwaka mmoja kabla.
Uchambuzi wa Karl Zawadzky,mnasimuliwa studioni na Ramadhan Ali:
Hali ya kufurahisha kabisa katika soko la kazi ambayo kwa jicho la hali mbaya iliokuwapo yamfanya mtu kuieleza sasa ni miujiza. Sababu zake ni 2:
Sababu ya kwsanza ni kufufuka uzuri kwa uchumi wa Ujerumani kumesababisha nafasi zaidi za ajira na kupungua kwa ukosefu wa kazi.Pili, mageuzi yaliofanywa katika soko la kazi yameanza kuuma au kufanya kazi.haya ni mageuzi aliyoyaanzisha Kanzela wa zamani Gerhard Schröder .Katika afisi za Leba ,kuajiri watu kunakwenda haraka-haraka na kwa njia zilizo bora.
Isitoshe, ikiwa mtu hana kazi na kaka tu bila ya kutafuta kazi, anapunguziwa ruzuku za wasio na kazi.Isitoshe, wale wasio na kazi kitambo kirefu,msaada waliokuwa wakipewa unapungua na hii inawafanya waache uvivu na kurudi makazini.
Lakini bila kustawi kwa uchumi,mageuzi yaliofanywa katika soko la kazi yasingefanya kazi .Kustawi kwa uchumi kunachangia nako viwanda kuzalisha bidhaa kupiota kiasi nah ii inavifanya kuajiri zaidi wafanyikazi.
Wakati miaka 2 nyuma kulikuwapo nafasi 420,000 za kazi katika mashirika ya kuajiri kazi,hivi sasa nafasi hizo zimeongezeka na kuwa 920,000.
Katika mikoa na matawi ya viwanda upungufu wa wafanyikazi umeshageuka kizuizi kwa uchumi kuzidi kukua na kuimarika.Hasa wahandisi na mabingwa wa komputa ndio wanaosakwa zaidi na kuna upungufu.
Inaonesha kwa mara nyengine tena: kukua kwa uchumi sio turufu,lakini bila uchumi kukuwa ,hakuna turufu.Kwa lugha nyengine,kwa kukua kwa uchumi matatizo mengi ingawa sio yote,huweza kupatiwa ufumbuzi.
Kwa mfano, mfuko wa ruzuku kwa wasio na kazi wa Idara ya Leba baada ya kupita miaka mingi ya kasoro sawa na mfuko wa bima ya wasio na kazi,sasa mifuko hiyo imejaa na hata kupindukia.Hii maana yake, waziri wa fedha wa Ujerumani mwaka huu ametia mfukoni kodi ya mapato inayopindukia bilioni 10 na fedha hizo zinapindukia makisio.
Kutokana na kustawi uchumi na kuzidi watu kupata ajira,wizara za fedha zinaongeza mapato ya kodi na bima za uzeeni nazo zinazidi kutia fedha.hata wanunuzi wa kibinafsi madukani nao wameaanza kutumia badala ya kubana matumizi kama ilivyokuwa hapo kabla.Kwa ufupi,baada ya dhiki si dhiki,badaa ya dhiki faraji.
Ni wazi sasa watu wanahisi upepo mpya unavuma na manunguniko yanaanza kupungua.
Hali hii, yapasa sasa kuwatia shime wanasiasa kuitumia hali bora katika soko la kazi kuzidi kuutia jeki uchumi na kupunguza zaidi ukosefu wa ajira.Kwani, kuna mengi bado ya kutenda !