1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hujuma kwenye Nord Stream bado kitendawili

26 Septemba 2023

Mwaka mmoja uliopita milipuko iliharibu sehemu muhimu ya miundombinu ya nishati ya Ulaya. Licha ya uchunguzi unaoongozwa na serikali na waandishi wa habari, bado haijulikani hadi sasa muhusika wa hujuma hizo.

https://p.dw.com/p/4Wnnf
Picha iliyosambazwa na serikali ya Denmark Septemba 27, 2022 kionyesha namna gesi ilivyokuwa ikimwagika katika bomba la Nord Stream
Picha iliyosambazwa na serikali ya Denmark Septemba 27, 2022 kionyesha namna gesi ilivyokuwa ikimwagika katika bomba la Nord Stream Picha: Danish Defense Ministry/Xinhua/picture alliance

Milipuko ya Septemba 26, 2022 iliyoharibu mabomba ya Nord Stream ilikata njia kuu ya usafirishaji wa gesi kutoka nchini Urusi hadi Ulaya na kuchochea mivutano ya kimaeneo ambayo tayari ilikuwa imeshamiri kutokana na uvamizi wa Moscow nchini Ukraine.

Lakini mwaka mmoja baada ya milipuko hiyo na licha ya kufanyika uchunguzi katika nchi tatu, swali la nani aliyehusika na kitendo hicho cha hujuma bado halijapata jibu. Kwa kukosekana na ushahidi wa kutosha, nadharia tofauti zimeibuka zikinyooshea kidole Ukraine, Urusi au Marekani. Hawa wote wamekana kuhusika.

Soma pia:Marekani: Mripuko wa mabomba ya Nord Stream ilikua hujuma 

Mwishoni mwa Septemba mwaka 2022, kulifanyika mfululizo wa milipuko ya chini ya maji iliyopasua mabomba matatu kati ya manne yanayounda mradi wa Nord Stream 1 na Nord Stream 2, yaliyokuwa yakisafirisha gesi kwenye Bahari ya Baltiki.

Soma pia:Viongozi walaumu hujuma kwa uvujaji wa Nord Stream 1 na 2 

Kampuni kubwa ya nishati ya Urusi, Gazprom mwezi Agosti tayari ilikuwa imesitisha usafirishaji wa gesi katika bomba la Nord Stream 1, iliyokuwa njia kuu ya kusafirisha gesi asilia kutoka nchini Urusi hadi Ujerumani, katikati ya mizozo iliyochochewa na vita vya nchini Ukraine.

Mabomba ya Nord Stream 2 yaliyokuwa yanayopokea gesi kutokea Urusi, yaliyoko katika mji wa Lubmin, kaskazini mwa Ujerumani
Mabomba ya Nord Stream 2 yaliyokuwa yanayopokea gesi kutokea Urusi, yaliyoko katika mji wa Lubmin, kaskazini mwa UjerumaniPicha: Michael Sohn/AP

Mradi wa Nord Stream 2 ulipingwa vikali na Ukraine na magharibi.

Mabomba ya Nord Stream 2 hayakufunguliwa wakati Berlin ikiachana na mradi huo siku kadhaa kabla ya majeshi ya urusi hayajaingia Ukraine, Februari 24,2022. Mradi huo wa thamani ya yuro bilioni 10 kwa muda mrefu ulipingwa na Ukraine, Marekani na mataifa ya Ulaya kutokana na hofu kwamba utaifanya Urusi kuwa na ushawishi zaidi kwenye usalama wa nishati nchini Ujerumani.

Denmark na Uswisi ziliungana na Ujerumani kufanya uchunguzi wa mashambulizi hayo kwa kuwa gesi ilivuja katika kanda huru za kiuchumi. Hata hivyo nchi zote tatu zimekuwa waangalifu katika kuzungumzia matokeo ya uchunguzi wao, jambo ambalo wachambuzi wanasema halishangazi kutokana na hofu ya kidiplomasia kutokana na kile wanachoweza kufichua.

Soma pia:Uingereza yakanusha madai ya kuhujumu mabomba ya gesi 

Hata hivyo, Idara ya ujasusi ya kijeshi ya Uholanzi ililieleza Shirika la ujasusi la nchini Marekani, CIA juu ya mpango wa Ukraine wa kulipua mabomba hayo miezi mitatu kabla ya shambulio hilo, hii ikiwa ni kulingana na shirika la utangazaji la Uholanzi NOS, gazeti la Die Zeit la Ujerumani na shirika la utangazaji la ARD, mnamo mwezi Juni. Gazeti la Washington Post la Marekani pia lilitoa madai kama hayo.

Lakini rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky ameyakanusha mara kwa mara madai hayo.

Kulingana na New York Times, maafisa wa Marekani waliona viasharia vya kijasusi vilivyoshiria kwamba kundi lililo nyuma ya Ukraine lilihusika na mashambulizi hayo bila ya Zelensky kujua.

Picha hii iliyotolewa Septemba 29, 2022  na vikosi vya Denmark inaonyesha eneo la maji ambako chini yake kulivuja gesi baada ya mabomba ya kusafirisha gesi kushambuliwa.
Picha hii iliyotolewa Septemba 29, 2022 na vikosi vya Denmark inaonyesha eneo la maji ambako chini yake kulivuja gesi baada ya mabomba ya kusafirisha gesi kushambuliwa.Picha: Rune Dyrholm/Armed Forces of Denmark/AP/picture alliance

Nani anayehusika na mashambulizi haya?

Waandishi wa habari wa gazeti la Der Spiegel la Ujerumani na shirika la utangazaji la ZDF waliandika kwamba mashambulizi yalifanywa na kikundi cha watu sita. Taarifa zilisema walitumia pasi za kughushi kukodisha mashua na malipo ya kukodisha yalifanywa na kampuni iliyosajiliwa Poland yenye uhusiano na mwanamke mmoja wa mjini Kyiv.

Soma pia: Sweden yasema bado haijulikani ni nani aliyehujumu bomba la gesi la Nord Stream 2

Tofauti na wao, vyombo vya habari vya Denmark viliripoti kuwa manowari ya jeshi la maji la Urusi chapa SS-750, ilipigwa picha ikiwa karibu na eneo kulipotokea milipuko siku chache kabla ya shambulizi hilo.

Madai ya mwandishi wa habari za upelelezi wa Marekani Seymour Hersh kwamba Marekani ilihusika na mashambulizi hayo ikisaidiwa na Norway yalipingwa na ikulu ya White House na kuyaita "ya kubuni".

Lakini wataalamu kama Andreas Umland, mchambuzi katika Kituo cha Mafunzo ya Ulaya Mashariki huko Stockholm anasema upo uwezekano mkubwa kwamba Urusi inahusika.

Shutuma dhidi ya Kyiv zinaweza kutishia msaada wa washirika, ambayo itakuwa na manufaa kwa Urusi. Amesema madai kwamba Ukraine ilihusika yangesababisha kuharibu msaada wa magharibi na kuwa na faida kubwa kwa Urusi.

Wakati huo huo, mabomba yaliyoharibiwa yanaweza kusaidia Gazprom kuepuka madai ya fidia ya gesi ambayo haikusafirishwa, ingawa kampuni hiyo ilionyesha kusita kuyafungua mabomba kabla ya milipuko hiyo.

Moscow pengine ilikuwa inataka "kuua ndege wawili kwa jiwe moja", alisema Umland.

Kremlin yenyewe imekanusha vikali kuhusika.