Ukeketeji kuadhibiwa kisheria Ujerumani
12 Februari 2010Uhalifu wa ukeketaji utapaswa kufuatiliwa kwa mujibu wa sheria ya Ujerumani ikiwa alietendewa anaishi nchini Ujerumani.
Kwa muda mrefu mashirika yanayotetea haki za wanawake yamekuwa yanapigania kupitishwa kwa sheria nchini Ujerumani , dhidi ya ndoa za kulazimishwa na dhidi ya kuwatahiri vigori.
Baraza la wawakilishi limepitisha mswada wa sheria ya kuadhibu uhalifu wa ukeketaji na ndoa za kulazimisha.
Waziri wa sheria wa jimbo la Hesse Jörg Uwe Hahn amesema kwenye Baraza la wawakilishi leo kwamba ukeketaji ni ukatili mkubwa wanaofanyiwa wanawake na wasichana. Waziri huyo ameeleza kuwa wanawake na wasichana wanaofanyiwa ukatili huo wanaishi na majeraha ya daima, katika mwili na moyoni.
Shirika linalotetea haki za wanawake Terre des femme limeunga mkono mswada uliowasilishwa na majimbo ya Ujerumani.
Hapo awali kosa la kumkeketa msichana lilizingatiwa kuwa ni kitendo cha hatari cha kumdhuru mtu tu.Adhabu yake ilikuwa kifungo cha miezi sita jela.
Lakini sasa mswada wa sheria uliowasilishwa na wawakilishi wa majimbo unataka itolewe adhabu ya kifungo cha kuanzia miaka miwili jela.
Uhalifu huo unafanyika hasa barani Afrika, lakini unafanyika pia katika nchi fulani za Asia na Amerika ya kusini. Hatahivyo nchini Ujerumani pia uhalifu huo unatendeka. Kwa mujibu wa takwimu za mashirika ambayo si ya kiserikali wanawake wapatao alfu 20 wamefanyiwa ukatili wa kukeketwa nchini Ujerumani.
Baraza la wawakilishi pia kwa mara nyingine limetaka kupitishwa kwa sheria na bunge la Ujerumani ya kuadhibu ndoa za kulazimishwa.
Chini ya sheria hiyo, ikipitishwa na bunge, mhalifu atapewa adhabu ya kifungo jela , kuanzia miezi sita.
Mwandishi: Bernd Gräßler
Tafsiri: Abdu Mtullya
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman