1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukeketaji wa wanawake: Waathiriwa elfu 68 Ujerumani

25 Juni 2020

Wizara ya familia nchini Ujerumani inakadiria idadi ya waathiriwa wa ukeketaji wa wanawake nchini humo imeongezeka kwa asilimia 44 kutoka mwaka 2017 na karibu wasichana elfu 15 huenda wanakabiliwa na hatari ya mila hiyo.

https://p.dw.com/p/3eKjo
Deutschland Familienministerin Franziska Giffey
Picha: Reuters/H. Hanschke

Ripoti ya wizara ya familia nchini Ujerumani inakadiria kuwa idadi ya waathiriwa wa ukeketaji wa wanawake nchini Ujerumani imeongezeka kwa asilimia 44 kutoka mwaka 2017 na karibu wasichana elfu 15 huenda wanakabiliwa na hatari ya mila hiyo. Waziri wa wizara hiyo Franziska Giffey, amesema ongezeko hilo linatokana na wimbi la wahamiaji.

Giffey ametangaza Alhamisi kuwa idadi ya wanawake na wasichana nchini humo ambao wamepitia kadhia hiyo ya ukeketaji imeongezeka kufikia elfu 68. Ongezeko hilo la asilimia 44 kutoka idadi ya mwisho iliyokadiriwa mwaka 2017 ilihusishwa na uhamiaji mkubwa kutoka mataifa ambapo ukeketaji wa wanawake ni jambo la kawaida.

Athari za ukeketaji

Giffey amewaambia waandishi wa habari kuwa ukeketaji wanawake ni ukiukaji mkubwa wa haki za kibinadamu na uhalifu wa jadi unaokiuka haki za wasichana na wanawake na pia uadilifu wa mwili na uamuzi wa kijinsia. Giffey ameongeza kwamba utamaduni huo una athari za maisha za kimwili na kisaikolojia kwa waathiriwa.

Waziri huyo amesema lengo lake ni kuwalinda wasichana na wanawake dhidi ya ukeketaji na kuwapa usaidizi.

Hatua mpya za kuwahamasisha wanawake

Giffey alitoa wito wa mikakati mipya katika jamii za maeneo kuzuia idadi hiyo kuongezeka zaidi.Mwenyekiti wa kundi la kutetea haki za binadamu Nala Fadumo Korn, amesema lengo sasa linapaswa kuwa kuwahamasisha akina mama kuwalinda watoto wao. Aliwasilisha ombi la sahihi elfu 125 dhidi ya ukeketaji kwa Giffey.

Giffey amesema ongezeko hilo kutoka idadi ya elfu 44 mwaka 2017 lilikuwa kubwa mno kwa sababu ya ongezeko la uhamiaji kutoka kwa mataifa kama Eritrea, Somalia, Indonesia, Misri na Nigeria.Shirika la afya duniani linakadiria kuwa takriban wanawake milioni 200 na watoto kote duniani wamepitia ukeketaji.