Ukeketaji: desturi haramu inayoendelea
Japokuwa umepigwa marufuku, ukeketaji bado unafanyika katika nchi nyingi za Afrika. Wasichana wa kipokot ni miongoni mwa wasichana wengi duniani ambao wanateseka licha ya desturi hiyo kupigwa marufuku nchini Kenya.
Wembe mmoja hutumiwa kwa wote
Mkeketaji huyu katika kanda ya bonde la ufa nchini Kenya ameshawakeketa wasichana wanne. Wembe alioutumia ni mmoja tu. Tendo hilo la kikatili katika desturi za kipokot linadhihirika wakati ambapo wasichana wanageuka kuwa wanawake. Ukeketaji unakatazwa katika nchi nyingi, ikiwemo Kenya. Hata hivyo, unaendelea - na zaidi katika maeneo ya wafugaji, mbali na miji.
Maandalizi ya sherehe
Wanawake na watoto wa kipokot wanaota moto ili kujikinga dhidi ya baridi ya asubuhi huku wakisubiri sherehe ya ukeketaji kuanza. Ni vigumu kwa wanawake wasiokeketwa kuolewa. Katika maeneo ya mbali na miji kuolewa ni muhimu. Kunawawezesha wanawake kukubaliwa katika jamii na kupata riziki. Msichana anayekataa kukeketwa anakuwa hatarini kutengwa na jamii.
Hakuna njia ya kukataa
Kabla ya kukeketwa, wasichana wanavuliwa nguo zao na kusafishwa kwa maji. Wanayotarajia maishani wanayajua: Kama vile mama zao, watateseka kimwili, kuanzia uvimbe na maambukizo ya kila aina mpaka utasa na matatizo wakati wa kujifungua. Ukeketaji unafanyika katika nchi 28 duniani, zikiwemo nchi za Afrika, Asia na Arabuni. Hata binti za wahamiaji barani Ulaya wapo hatarini.
Kungoja kwa wasiwasi
Wasichana wanangojea sherehe ya ukeketaji huku wakijawa na wasiwasi. Sheria ya Kenya imekataza ukeketaji tangu mwaka wa 2011. Takwimu za Shirika la kimataifa la kuwasaidia watoto zinaonyesha kuwa asilimia 27 ya wanawake wa Kenya wenye umri wa miaka 15 hadi 49 wamekeketwa. Mara nyingi wasichana hukeketwa bila ya kuwatia ganzi, kwa kutumia vyombo visivyosafishwa. Mwisho wake ni mateso yanayodumu.
Hatari ya kupoteza maisha
Mkeketaji akifanya kazi yake, msichana ana wajibu wa kuwa shupavu, na wala hawaruhusiwi kulia. Shirika la afya duniani linakadiria kuwa asilimia 10 ya wasichana wanafariki wakati wa kukeketwa, na asilimia nyingine 25 wanapoteza maisha yao baadaye kutokana na tendo hilo. Huenda idadi ya wanaokufa ikazidi hapo. Nchini Somalia, asilimia 98 ya wanawake wamekeketwa.
Jiwe lililotapakaa damu
Aina za ukeketaji zinatofautiana kulingana na makabila ya watu. Shirika la afya duniani WHO limebainisha aina tatu za ukeketaji, ambazo zinahusisha kuondoa kabisa sehemu fulani za uke au kuzipunguza.
Uchoraji miili katika rangi nyeupe
Kufuatia desturi za wapokot, wasichana wanachorwa rangi nyeupe. Wasichana hufariki kutokana na kupoteza damu nyingi. Nchi nyingi zimeanzisha harakati za kutoa elimu kuhusu mambo hayo. Hata hivyo, harakati hizo huhitaji muda mrefu ili kuleta mabadiliko. Kenya ina kitengo maalumu cha polisi cha kufuatilia kesi za ukeketaji. Raia wanaweza kupiga nambari maalumu ili kuripoti vitendo hivyo.
Kiwewe cha maisha
Baada ya kukeketwa, wasichana wanavishwa ngozi za ng’ombe na kuondolewa katika hali ya kiwewe. Kidesturi, wapo tayari kuolewa kuanzia wakati huo, na kwa mahari makubwa. Baadhi ya jamii zinaamini kuwa ukeketaji unaongeza usafi wa mwili, kwamba wanawake waliokeketwa ni waaminifu zaidi. Madhara yanayofuatia ukeketaji huo hayawezi kuondolewa hata kwa upasuaji wa kisasa.
Kutoka kwa mama hadi kwa binti?
Msichana huyu kamwe hatasahau ukatili alioupitia maishani mwake. Je, akishazaa binti, ataweza kumwepusha desturi hiyo? Kuna baadhi ya nchi ambako watoto wadogo wanafanyiwa ukeketaji. Sababu yake ni kutaka kulificha tendo hilo haramu: Mtoto mchanga anayelia pasipo kuacha ni kawaida tu na wala hazui tuhuma.