Ukeketaji bado waota mizizi Kenya
30 Mei 2006Mpango wa pamoja wa wizara ya afya nchini Kenya na shirika la maendeleo la Ujerumani GTZ una azma ya kutafuta suluhisho la kudumu juu ya kitendo cha ukeketaji.
Kajiado wilaya ilio kusini magharibi mwa Kenya ni sehemu ambako shughuli za ukeketaji wanawake bado zimeshika hatamu na jamii ya eneo hilo bado hata haionyeshi dalili za kutaka kuachana na mila na tamaduni hiyo.
Hata hivyo wilaya ya Kajiado ndio umetengwa kwa mpango wa mdahalo wenye lengo la kupiga mbiu dhidi ya vitendo vya ukeketaji.
Wizara ya afya na shirika la maendeleo la Ujerumani Deutsche Gesellschaft für Technische Zusammenabeit zinashirikiana katika kujenga mdahalo ambao unaihusisha jamii kuzungumzia madhara mbali mbali yanayoweza kusababishwa na ukeketaji.
Takwimu za serikali katika ngazi ya kitaifa zinaonyesha kuwa asilimia 32 ya shuguli za ukeketaji bado zianendelea nchini Kenya lakini hali hiyo inaonyesha kuwa katika kiwango cha juu cha asilimia 90 katika wilaya ya Kajiado pekee.
Bibi Phoebe Mollel mratibu wa mpango huo wa kupambana na ukeketaji katika wilaya ya Kajiado amesema kwamba hapo awali ilikuwa vigumu kuishawishi jamii ya wamaasai kuhudhuria mikutano iliyojadili ukeketaji hivyo basi mradi uliwajibika kutumia mbinu zingine kama vile kujadili katika mdahalo athari za ugonjwa wa ukimwi na maradhi ya zinaa.
Uchunguzi uliofanywa mwaka jana na wizara ya afya kwa ushirikiano na shirika la Ujerumani la GTZ ulionyesha kuwa asilimia 93.9 ya wasichana na wanawake kutoka jamii ya wamaasai walikeketwa hali ambayo iliwajibisha juhudi za kila aina kufanywa ili kuendeleza kampeni dhidi ya ukeketaji.
Juhudi za kupambana na kitendo cha ukeketaji kinacho mdhulumu mwanamke kwa njia moja au nyingine zimeanza kuzaa matunda katika wilaya ya Kajiado.
Mdahalo baina ya jamii ya wamaasai dhidi ya ukeketaji ulianza mwaka uliopita katika kata tatu kati ya saba zilizopo wilayani Kajiado na kufanikiwa kwa mpango huu kumefungua mlango hadi kufikia mkoa wa mashariki ambao pia umeathiriwa vibaya na ukeketaji nchini Kenya.
Bibi Mary Kiluso, Ngariba aliyehusika na kuwakeketa wasichana ni mfano wa kuigwa kwani aliamua kuacha kazi yake hiyo pamoja na kuwa ilikuwa inampa kipato cha takriban dola 14 kwa kila msichana au mwanamke aliyepita chini ya kisu chake.
Bi Kiluso ambae pia ni mkunga wa kienyeji ameliambia shirika la habari la IPS kwamba ukeketaji unasababisha madhara mengi hasa wakati wa kujifungua na wengine wengi kushindwa kuketi vyema baada ya kukeketwa.
Katika mila za kimaasai msichana akishakeketwa basi hiyo ni ishara kuwa yuko tayari kuolewa hatua ambayo Bi kiluso anasema anajuta kuwa alichangia ndoa za mapema tangu alipoanza shughuli yake hiyo mwaka 1970.
Mbali na madhara chungu nzima yanayosababishwa na ukeketaji hatua hiyo pia inamnyima raha ya kufanya mapenzi mwanamke aliyekeketwa vile vile maambukizi ya virusi vya ukimwi kutokana na visu na vifaa vingine vinayvotumika wakati wa shughuli ya ukeketaji.
Kwa mujibu wa shirika la kutetea haki za binadamu Amnesty International zaidi ya nchi 28 zinaendeleza shughuli za ukeketaji barani Afrika.
Wenige wanao endeleza ukeketaji wanafanya hivyo kwa kuamini kuwa hiyo ndio njia moja ya kuuvua ujana na kuingia katika utu uzima au kuipa sura ya kupendeza sehemu ya siri ya mwanamke.