Tangazo la Balfour bado mwiba mchungu Mashariki ya Kati
2 Novemba 2017Katika taarifa ya maneno 67 ilioandikwa miaka 100 iliyopita, Uingereza iliidhinisha kuwekwa makaazi ya Wayahudi katika kanda ya Mashariki ya Kati, na kuanzisha mchakato ulioishia katika kuundwa kwa taifa la Israel, na pia mmoja ya migogoro migumu zaidi kushughulikia.
Viongozi wa Uingereza na Israel, hii leo wanaadhimisha karne moja ya taarifa hiyo, inayojulikana kama "Tangazo la Balfour" kufuatia jina la waziri wa mambo ya nje alieiandika - Arthur Balfour - kwa karamu ilioandaliwa katika ukumbi wa jumba la Lancaster mjini London.
Lakini wakati waziri mkuu Theresa May na Benjamin Netanyahu wakiadhimisha siku hii, waandamanaji mjini London and katika maeneo ya Wapalestina, wanaandamana kuishinikiza Uingereza ikiri kuhusu mateso ambayo wanasema yamesababishwa na tangazo hilo kwa watu wa Palestina, na kutambua haki yao ya kuwa na taifa huru.
Adnan Hussein, gavana wa Kipalestina na mji wa Jerusalem, alisema baada ya kufikisha ujumbe wao kwa ubalozi mdogo waUingereza mjini humo, kuwa wanaitaka Uingereza ikiri juu mateso iliyoyasababisha kwa watu wa Palestina kupitia tangazo hilo.
"Tumemuambia mwakilishi tulichotaka kusikia kutoka kwa Uingereza, na tumemuambia kuwa hatufikirii kwamba katika kumbukumbu hii ya miaka 100 ya ahadi nyeusi, tunaitarajia Uingereza kukiri makosa na kulitambua taifa la Palestina, kilichotokea ni kutambua na kusherehekea miaka 100 ya mateso, hivyo tunatangaza hili kwa mwakilishi na tumemuambia afikishe ujumbe huu kwa serikali ya Uingereza," alisema Gavana huyo wa mji wa Jerusalem.
Furaha, majonzi Mashariki ya Kati
Wakati Israel inampa heshima kubwa Arthur Balfour, na kuiita mitaa na shule mjini Tel Aviv kwa majina yake, Wapalestina wanakosoa tangazo lake wakilitaja kama ahadi ya Uingereza kutoa ardhi ambayo haikuwa milki yake. Tangazo hilo linalobishaniwa ndiyo mzizi wa mzozo wa ardhi kati ya Waisrael na Wapalestina ambao, baada ya vita kadhaa na miongo ya diplomasia ya kimataifa, unaendelea kukosa ufumbuzi.
Uingereza iliishikilia Palestina, ambayo awali ilikuwa chini ya utawala wa himaya ya Ottoman ya Waturuki, kuanzia mwaka 1922 hadi baada ya kumalizika kwa vita kuu vya pili vya dunia. Israel iljitangazia uhuru mwaka 1948, mwishoni mwa utawala wa laazima wa Uingereza, na baada ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kupiga kura mwaka 1947, kuunga mkono mpango uliokataliwa na wawakilishi wa Wapalestina, kuigawa Palestina kati ya taifa la Kiyahudi na la Kiarabu.
Mgogoro wa kikanda uliyofuatia hatua hiyo, ambao umehusisha vita kadhaa vilivyopiganwa kati ya Waarabu na Waisrael, umewaacha Wapalestina wakitafuta kuunda taifa huru katika maeneo yaliotekwa na Israel wakati wa vita vya Mashariki ya Kati vya mwaka 1967.
Rais wa Mamlaka ya ndani ya Wapalestina Mahmoud Abbas alitumia makala alioiandika katika gazeti la Uingereza la Guardian, kurudia wito wake kwa serikali ya Uingereza kukiri kwamba tangazo hilo lilikuwa kosa. Uingereza imekata madai ya huko nyuma ya Palestina ikiitaka kuomba radhi, na zaidi ya hayo, haiitambui rasmi Palestina kama taifa.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre,dpae,ape.
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman