Ujumbe wa Wakfu wa Jimmy Carter kwa Kenya wakati wa uchaguzi
7 Agosti 2017Wakfu wa Jimmy Carter, rais wa zamani wa Marekani, leo umewasilisha ujumbe muhimu kwa Kenya wakati nchi hiyo ya Afrika Mashariki ikijiandaa kufanya uchaguzi mkuu hapo kesho. Ujumbe huo umewasilishwa na aliyekuwa Waziri wa Mashauri ya Nchi za Nje wa Marekani, John Kerry.
Bwana Kerry, ambaye anaongoza ujumbe wa waangalizi wa kimataifa kutoka wakfu wa Carter, amepongeza jitihada za Mahakama kuu nchini katika kujiandaa kushughulikia kesi zozote ambazo huenda zikajitokeza kabla, wakati na baada ya uchaguzi mkuu. Kerry amesema: "Nimefurahi sana kuwa miongoni mwa waangalizi wa kimataifa kuwa humu nchini Kenya kusaidia Wakenya kwa imani kuwa uchaguzi huu mkuu utakuwa wa haki na huru. Ningependa kuishukuru idara ya mahakama kwa kazi nzuri ambayo tayari wamefanya kuhakikisha wanasuluhisha kesi zinazoibuka wakati na baada ya uchaguzi wa kesho."
John Kerry ambaye ni waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Marekani, pia ameandamana na Bi Aminata Toure, aliyekuwa waziri mkuu wa Senegal.
Bi Toure amesema Kenya ni mfano bora wa mataifa ya bara hili ambayo yanatoa mwamko mpya wa demokrasia na akatoa ombi kwa Wakenya kujitokeza kwa wingi hapo kesho kupiga kura na kuzingatia amani wakati wa mchakato wa zoezi la uchaguzi. Bi Toure ameongeza kuwa "Tuna hakika ifikapo hapo kesho itakuwa fursa muhimu ya kushuhudia kwamba hali ya kidemokrasia nchini Kenya kwa kweli imekomaa na Wakenya wanaweza kujitokeza kupiga kura kwa njia ya haki na amani. Na hilo litakuwa jambo la kujivunia sisi kama Waafrika."
Mahakama iko tayari kusuluhisha kesi zitakazowasilishwa
Kwa upande wake, Jaji Mkuu wa Kenya, David Maraga kwa mara nyingine tena amewahakikishia Wakenya na jumuiya ya kimataifa kwa jumla kuwa idara yake ya mahakama kuu ipo tayari kutatua kesi zozote zitakazowasilishwa kortini kabla, wakati na baada ya uchaguzi mkuu. Amesema,"Idara yetu ya mahakama ipo tayari kushughulikia malalamishi yoyote kuhusu uchaguzi. Tayari tumeshughulikia kesi zote zilizowasilishwa kabla ya uchaguzi. Na tuko tayari kukabiliana na kesi nyingine endapo zitawasilishwa kortini, kwa hivyo hamna wasiwasi wowote."
Ujumbe wa wakfu wa Carter utawatuma zaidi ya waangalizi wapatao 50 katika vituo mbalimbali vya kupigia kura kote nchini ifikapo hapo kesho.
Wakati hayo yakijiri, hali ya usalama imeimarishwa kote nchini, huku idara ya usalama ikidokeza kuwa imeshawatuma maafisa wake wasiopungua 180,000 kushika doria katika vituo vya kupigia kura kote nchini.
Uchaguzi mkuu wa hapo kesho unatazamiwa kuwa na ushindani mkali baina ya Rais Uhuru Kenyatta, mgombea wa chama tawala cha Jubilee, anayepigania muhula wa pili dhidi ya mpinzani wake mkuu Raila Odinga, kinara wa muungano wa upinzani, NASA.
Rais Kenyatta mwenye umri wa miaka 55, ni mtoto wa aliyekuwa rais wa Kwanza wa Kenya, Mzee Jomo Kenyatta, ilhali Odinga, mwenye umri wa 72, ni mwana wa aliyekuwa Makamu wa rais wa kwanza, Jaramogi Oginga Odinga. Zaidi ya Wakenya wapatao milioni 19 wamesajiliwa kama wapiga kura katika uchaguzi wa mwaka huu.
Mwandishi: Reuben Kyama/DW Nairobi
Mhariri: Mohammed Khelef