Ujumbe wa UN wakutana na pande hasimu Yemen
27 Desemba 2018Maafisa wa Yemen wamesema wajumbe wa Umoja wa Mataifa wanaosimamia utekelezaji wa makubalinao ya kusitisha mapigano katika mji wa bandari wa Hodeida kwa mara ya kwanza wamekutana na wawakilishi wa pande zinazopigana katika vita vya nchini Yemen.
Ujumbe wa Umoja wa Mataifa unaoongozwa na meja jenerali wa Uholanzi Patrick Cammaert uliwasili katika mji huo wa bandari mwishoni mwa wiki iliyopita. Mazungumzo ya pande mbili hizo yalihusu taratibu zinazotumiwa na ujumbe wa Umoja wa Mataifa katika kutekeleza amri ya kusimamisha mapigano na pia juu ya idadi ya waangalizi watakaohitajika katika siku zijazo.
Meja jenerali Patrick Cammaert, anaongoza kamati ya pamoja, ambayo inajumuisha pande zote mbili za viongozi wa serikali na waasi wa Houthi, katika mkutano wake wa kwanza wa ana kwa ana na wawakilishi hao. Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane Dujarric ameelezea kuwa mkutano huo ni mojawapo ya vipaumbele vya ujumbe wa Cammaert.
Pande zinazopigana nchini Yemen zilifikia makubaliano ya kusitisha mapigano kwenye mazungumzo ya amani ya nchini Sweden yaliyofanyika mwezi wa Desemba. Hatua ya kusimamisha mapigano katika mji wa Hodeida ilianza kutekelezwa katika mji huo na kwenye vitongoji vyake tarehe 18 mwezi huu lakini hali bado haijakuwa thabiti. Kila upande umedai kuwa upande mwingine umeyakiuka makubaliano.
Kwa mujibu wa ripota wa shirika la habari la AFP, majeshi ya serikalai ya Yemen yanayosaidiwa na mfungamano wa kijeshi unaoongozwa na Saudi Arabia yalipambana na waasi wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran kwa muda wa saa chache hapo Jumatano asubuhi.
Afisa wa upande wa majeshi ya umoja unaoongozwa na Saudi Arabia amefahamisha kwamba mnamo siku ya Jumatatu askari wake10 waliuawa tangu amri ya kusimamisha mapigano ilipoanza kufanya kazi, akiwashutumu wapiganaji wa Houthi kwa kukiuka mara 183 makubaliano hayo. Waasi, kwa upande wao, wamesema siku hiyo hiyo waliorodhesha ukiukaji wa makubaliano hayo mara 31uliofanywa na vikosi vya serikali katika kipindi cha saa 24.
Katika kadhia nyingine maafisa wa Yemen wamesema watu wapatao 17 waliuawa kutokana na mapigano baina ya majeshi ya serikali na waasi wa Houthi yaliyotokea mnamo siku mbili zilizopita katika mji mkuu wa Yemen, Sanaa. Idadi hiyo inajumuisha watu waliouawa kutoka pande zote mbili.
Mwandishi:Zainab Aziz/APE/AFP
Mhariri:Josephat Charo