Ujumbe wa NATO Afghanistan hatarini?
5 Februari 2008Condoleezza Rice anatazamia kukutana na Waziri Mkuu Gordon Brown na Waziri wa Nje David Miliband wa Uingereza siku ya Jumatano mjini London.Uingereza ni mshirika mkuu wa Marekani na imeunga mkono mito ya Washington kupeleka vikosi zaidi katika maeneo ya mapigano kusini mwa Afghanistan. Marekani na Uingereza zinayashinikiza madola shirika kujitahidi zaidi kupiga vita,uasi wa Wataliban.Marekani na Uingereza zinayashinikiza madola shirika kujitahidi zaidi kupiga vita,uasi wa Wataliban.
Maafisa wa Kimarekani wamesema,hakuna uhakika wa kuwashinda Wataliban waliotimuliwa madarakani na vikosi vilivyoongozwa na Marekani nchini Afghanistan,zaidi ya miaka sita iliyopita.Hata mwandalizi wa Mkutano wa Usalama utakaofanywa mwishoni mwa juma hili mjini Munich kusini mwa Ujerumani amesema,kuna uwezekano kwa ujumbe wa NATO kushindwa nchini Afghanistan.
Marekani ikithibitisha kitisho hicho kikubwa,imesema Wataliban wanaofuata itakadi kali za Kiislamu,sasa wametupia jicho nchi jirani Pakistan inayoyumba.Kwa maoni ya Naibu Waziri wa Nje wa Marekani anaeshughulikia masuala ya Asia ya Kati na Kusini,mustakabali wa Afghanistan utakuwa hatarini ikiwa jumuiya ya kimataifa itaiipa kisogo nchi hiyo.Katika kampeni iliyowaudhi washirika wengi wa NATO,Marekani imesema washirika wake wanapaswa kujitolea zaidi kuwapiga vita Wataliban nchini Afghanistan.
Msemaji wa wizara ya nje ya Marekani,Sean McCormack alipozungumza na maripota mjini Washington siku ya Jumatatu alisema,washirika wa NATO wanapaswa kujitolea zaidi na kuimarisha idadi ya wanajeshi wake nchini Afghanistan.Lakini Uingereza,Kanada,Uholanzi na Denmark na hata Australia isiyo katika NATO zimesifiwa wazi wazi na Marekani kwa kuwajibika katika maeneo ya hatari kubwa mno huko Afghanistan.Marekani,ingependa kuona madola makuu ya Ulaya kama Ujerumani na Ufaransa yakijitolea zaidi kupigana katika maeneo yenye ngóme za Wataliban,kusini mwa Afghanistan.
Kwa mujibu wa gazeti la Kijerumani "Sueddeutsche Zeitung" Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani,Franz Josef Jung na Robert Gates wa Marekani,waliandikiana barua kali kufuatia mwito wa Marekani kuitaka Ujerumani ipeleke vikosi vya kupigana nchini Afghanistan.
Hivi sasa,zaidi ya wanajeshi 3,000 wa Ujerumani wanashiriki katika miradi mbali mbali ya ujenzi mpya kaskazini mwa Afghanistan,eneo lililo na utulivu wa aina fulani.Ujerumani licha ya kushinikizwa na NATO na Marekani,imepinga kupeleka vikosi vyake kusini mwa Afghanistan.Bila ya shaka suala hilo litakuwa na kipaumbele kwenye mkutano wa mawaziri wa ulinzi wa NATO utakaofanywa siku ya Alkhamisi katika mji mkuu wa Lithuania,Vilnius.