1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

-UJUMBE WA FIFA WAZURU AFRIKA KUSINI KUKAGUA MAANDALIO KWA KOMBE LA DUNIA LA KWANZA AFRIKA

30 Oktoba 2003
https://p.dw.com/p/CHYE

-NUSU-FINALI YA KOMBE LA KLABU BINGWA BARANI AFRIKA KATI YA USMA ALGIER NA ENYIMBA NAISMAILIA NA ESPERENCE
-NA WANARIADHA ZAIDI WAKENYA WAJITOLEA KUKIMBIA CHINI YA BENDERA YA NCHI NYENGINE

Natuanze na Bundesliga-Ligi ya Ujerumani: Mabingwa wa Ujerumani-Bayern Munich wanapaswa kucheza bora zaidi ikiwa wanataka kuepuka wasitoke mikono mitupu msimu huu.tayari katika orodha ya Ligi wameangukia nafasi ya 4 huku usukani wa Ligi ukibadilika mikononi mwa ama Bayer Leverkusen au Stuttgart na Bremen ikiwa nyuma yao.
Kati ya wiki hii, Munich nusra ivuliwe taji na mapema katika Kombe la taifa la Ujerumani ilipoweza kuitimua Nüremberg-klabu ya daraja ya pili kwa mikwaju ya kutoana ya penalty mwishoni mwa dakika 120.

Munich ilihitaji kipa wake Oliver kahn kuokoa mabao ya penalty mara 2 ili wasitolewe katika Kombe hilo la Taifa. Bayern munich imeanza msimu huu ikitumai kuseleleerza mamlaka yake nyumbani na kuyatumia kama jukwaa la kuparamia kileleni mwa vikombe vya ulaya na hasa Champions League-Kombe la klabu bingwa.Hii inafuatia kupigwa kumbo katika duru ya kwanza tu ya kombe hili msimu uliopita. Kujiimarisha kwa shabaha hiyo, munich ilimuajiri mshambulizi hatari Mholanzi Roy Makaay kutoka Deportivo la Coruna ya Spain,lakini pengine ilifanya makosa kumuuza mbrazil Giovanne Elber kwa Olympic Lyon ya Ufaransa.

Makaay amechangia hadi sasa mabao 6 lakini hii haikuzuwia Munich kusimama nafasi ya 4 na pointi 4 nyuma ya viongozi wa Ligi bayer Leverkusen,klabu ambayo nusra msimu uliopita iteremshwe daraja ya pili muda mfupi baada ya kuibuka makamo-bingwa tangu wa Kombe la klabu bingwa barani Ulaya hata wa Ujerumani-Bundesliga.

Msukosuko unaikumba pia klabu ya jiji kuu la Ujerumani-Hertha Berlin na kocha wake mholanzi Huub Stevens amepewa masharti ya kushinda mechi m bili zilizofuatia mpambano na Rostock wa mwisho wa wiki iliopita ama si hivyo akione kilichomtoa kanga manyoya. Stevens na kikosi chake waliilaza Rostock bao 1:0 jumamosi iliopita na siku 4 baadae,Berlin ikailaza tena Rostock katika Kombe la Taifa. Berlin lakini ilishinda kwa bahati tu,kwani Rostock na berlin zilirefusha mchezo na mwishoe kutoana kwa mikwaju ya penalty.Berlin ilivuka salama na hatima ya kocha wake Huub Stevens.

Mla lakini, wasema waswahili ni mla leo, mla jana kala nini.Ikiwa Stevens hatowika katika changamoto za Bundesliga mwishoni mwa wiki hii, basi shoka litarudi kumetameta kutaka kumfyeka. Klabu nyengine ya Ligi ya ujerumani inakabiliwa na kocha wake na balaa tofauti na lile la Bayern munich au Berlin:Kocha wa Schalke Juup Heynckes aliungama kati ya wiki hii kwamba amesangazwa na tofauti ya idadi kati ya wachezaji wa kijerumani na wale wa kigeni katika timu ya schalke na ameahidi kuigeuza sura hiyo.Schalke ina wachezaji 2 tu wenye pasi za kijerumani na waliosalia ni wageni.Wachezaji hao 2 ni Frank Rost kipa wao na Gerald Asamoah,mzaliwa wa Ghana aliechukua uraia wa Ujerumani.waliosalia wote hawana uraia wa Ujerumani.

Tatizo kama hili alilizungumzia karibuni kocha wa timu ya taifa ya ujerumani Rudi Völler.Schalke imeporomoka chini msimu huu na kocha Heynckes anaamini nidhamu inayoshikamanishwa na wajerumani imetoweka katika klabu ya Schalke.Iwapo Heynckes atafaulu kushinda kwa nidhamu tu yafaa kusubiri kuona.Alao mabingwa Bayern Munich na mashabiki wao hawajali idadi ya wachezaji wa kigeni katika safu yao,mradi tu akina Roy makaay kutoka Holland wanatia mabao na Bayern Munich inashinda.

Leo ni semi-finali ya pili ya Kombe la klabu bingwa barani Afrika-champions League kufuatia ile ya kwanza jana kati ya USMA Alger mjini Algiers,Algeria na Enyimba ya Nigeria.jioni hii zinapambana na mjini Ismailia,Misri.Ismailia na Esperence ya Tunisia. Esperence lazima ikomeshe dosari zake inapocheza na timu za Misri ama sihivyo, itaondoka mikono mitupu jioni hii.Utakumbuka kuwa, esperence ilitolewa na Al Ahly ya Misri kwa bao la ugenini kufuatia kutoka sare mara mbili katika nusu-finali ya mwaka 2001.Mwaka jana ilitolewa katika duru za kwanza baada ya kutoka sare nyumbani na kushindwa na zamalek mjini Cairo.

Mara pekee klabu hii ya tunis kutoroka na kombe la klabu bingwa barani afrika ilikua 1994 na walipojaribu kutetea taji lao hilo walizimwa tayari katika hatua ya robo-finali na walipolazwa nyumabni na kutoka sare nyumbani mwa Ismailia. Hakuna sababu lakini kwanini Esperence isikiuke kivuli chake na kuishinda leo Ismailia nyumbani mwao. Esperence ni timu pekee hadi sasa isioshindwa katika changamoto hizi-imeshinda mechi 6 na kutoka suluhu mara 4 katika mapambano dhidi ya Rayon sport ya Rwanda,Highlanders ya zimbabwe,canon yaounde ya Kamerun,USMA Alger ya Algeria na AS Aviacao ya Angola.

Ismailia ni mabingwa wa wa kombe hili 1969.Na si rahisi kuwatimua na hasa nyumbani,kwavile Ismailia imepata pigo moja tu wiki 2 nyuma ilipozabwa mabao 4-2 na Enyimba ya Nigeria,lakini ilitamba Ismailia mbele ya Zanaco ya zambia,Port Louis ya Mauritius ,Asec ya Ivory Coast na Simba ya Tanzania.

AFRIKA KUSINI NA KOMBE LA DUNIA 2010:
Juzi alhamisi Tume ya wakaguzi 5 wa FIFA-shirikisho la dimba ulimwenguni iliwasili Johannesberg,kwa ziara ya siku 7 ya kukagua uwezo wa Afrika Kusini kuandaa Kombe la kwanza la Dunia barani Afrika mwaka 2010.Wakaguzi hao 2 ni wabelgiji,mfinland mmoja, mfaransa na Mchili wanapewa heshima kama viongozi wa dola na mpango wa ziara yao umejumuisha mkutano na rais Thabo Mbeki jana.Leo ujumbe huo umezuru uwanja wa Ellis Park,uwanja uliochezewa finali ya Kombe la dunia la rugby 1995.Huko wanaangalia jioni hii robo-finali ya kombe la Ligi baina ya Kaizer Chief na Ajac Cape Town.

Tume ya wakaguzi wa FIFA imepangiwa pia karanu ya chakula cha usiku na Mfalme wa wazulu Goodwill Zwelithini mjini Durban pamoja na ziara katika kisiwa cha Roben Island nje ya pwani ya Cape town ambako Nelson Mandela aliwekwa korokoroni kwa kadiri ya miongo 3. Mzee Mandela akaja kuwa rais wa kwanza aliechaguliwa kidemokrasi nchini Afrika Kusini na wiki iliopita alikutana na rais wa FIFA Sepp Blatter huko Uswisi kutilia mkazo ombi la Afrika kusini kuandaa Kombe la dunia.Blatter amekuwa nyuma ya ombi la Afrika Kusini muda mrefu.

Baada ya kushindwa chupuchupu na Ujerumani kuandaa kombe la dunia linalokuja 2006,Afrika Kusini inaungwamkomno na vyombyo vyxa habari kote duniani kushinda dhidi ya wagombeaji wengine wa kiafrika-kura itakapopigwa April,mwakani.Wagombeaji hao ni Morocco,inayoleta kitisho kikubwa kwa afrika Kusini,Misri,Libya na Tunisia. Rais wa shirikisho la dimba la Ubelgiji Peeters alianza na tume yake ziara ya kuzikagua nchi hizo 5 zinazogembea kwa kuzuru kwanza Morocco mwezi huu na ameondoka huko amevutiwa mno na shauku kubwa na nia ya kushinda wapinzani ili kuandaa Kombe la kwanza la dunia.1994,Morocco ilishindwa kwa kura 4 tu na Marekani na imegombea mara 3 na kushindwa.

Afrika Kusini tayari ina zaidi ya viwanja 8 vinavyotakiw nchi kuwa navyo na ina mpango wa kuingeza viti katika uwanja wake maridadi wa Johannesberg kuchukua hadi mashabiki kutoka 80.000 hivi sasa hadi 110.000. Afrika Kusini ilipita mtihani wa kugombea kuandaa Kombe la dunia la 2006 lakini Mnew Zealand Charles Dempsey,alikuja kuitilia kitumba chake mchanga kwa kuzuwia kutoa kura yake na hivyo kuipa Ujerumani ushindi wa kura 12-11 za Afrika Kusini. Afrika Kusini imeahidi kufanya kila juhudi kuona inashinda mara hii.

TUMALIZIE RIADHA:
Mkenya mwengine anataka kukimbia chini ya bendera ya nchi nyengine badala ya Kenya : Gregory Konchellah, mtoto wa bingwa wa dunia wa zamani katika masafa ya mita 800 Billy Konchellah,amejiunga na safu ya wanariadha wa Kenya wanaobadilisha uraia kama vile Sammy Kipketer anaekimbia chini ya bendera ya Danmark au Seif Saeed Shaeen-alietwa zamani Stephen Cherono. Gregory Konchellah ameamua kukimbia chini ya bendera ya bahrein.Isaiah Kiplagat-mwenyekiti wa chama cha riadha cha Kenya amesema amepokea barua kutoka shirikisho la riadha ulimwenguni-IAAF ilimfungulia mlango Konchellah anaekimbia kama baba yake pia mita 88 kuiwakilisha Bahrein katika mashindano ya kimataifa katika michezo ya mwakani ya olimpik mjini Athens,Ugiriki.

Kiplagat amesema ameliandikia shirikisho la riadha ulimwenguni kutaka ufafanuzi zaidi.
Baadhi ya wanariadha mashuhuri wa Kenya wanakimbilia nchi za ulaya na nchi tajiri za ghuba kupata umaarufu zaidi na kunyanyua hali zao za kimaisha. Zaidi ya wakenya 10 wameshafanya hivyo wakiwakilisha mataifa tofauti wakati wa mashindano ya ubingwa wa riadha wa dunia mjini Paris, August mwaka huu.
Wanariadha 2 wengine wa Kenya Abel Cheruiyot na Leornard Mucheru wanaotaka pia kuiwakilisha bahrein,hawakupata bado idhini ya kufanya hivyo.