1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaNiger

Ujumbe wa ECOWAS watua Niger kutafuta suluhu

2 Agosti 2023

Ujumbe wa Jumuiya ya Kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi ECOWAS unaoongozwa na Nigeria, umewasili Niger kujadiliana na viongozi wa mapinduzi waliochukua madaraka wiki iliyopita.

https://p.dw.com/p/4UhAN
Afrika Nigeria Coup Demonstration
Picha: Fatahoulaye Hassane Midou/AP/picture alliance

Ujumbe huo uko Niamey wakati ambapo wakuu wa kijeshi wa jumuiya hiyo ya Afrika Magharibi wanakutana pia katika mji mkuu wa Nigeria Abuja.

Wakuu hao wa ulinzi wanaokutana huko Abuja kwa kipindi cha siku mbili, wanapanga mikakati ya jinsi ya kujibu mapinduzi hayo ya wiki iliyopita ambayo yameibua hofu ya mgogoro mpana katika kanda nzima ya Sahel huko Afrika Magharibi.

Nigeria yakata umeme wake Niger

Afisa mmoja mwandamizi wa jumuiya ya ECOWAS Abdel Fatau Musa aliyekuwa akizungumza baada ya kuanza kwa mkutano huo huko Abuja, amesema, jumuiya hiyo inaamini kuingia kijeshi Niger ili kumrudisha madarakani Rais Mohamed Bazoum aliyechaguliwa kidemokrasia, utakuwa ni uamuzi wa mwisho.

ECOWAS Meeting Afrika
Mfanyakazi wa ECOWAS akipita mbele ya meza ya kuandaa kikao na waandishi habariPicha: MICHELE SPATARI AFP via Getty Images

Afisa huyo lakini amesema kuwa ni sharti wajiandae kwa lolote lile litakalotokea.

Jumuiya hiyo iliiwekea Niger vikwazo vya kibiashara na kifedha Jumapili na sasa duru kutoka kampuni ya usambazaji umeme ya Niger inasema, Nigeria imesitisha usambazaji wa umeme kwa Niger chini ya vikwazo hivyo.

Huku ikiwa wiki moja tayari imepita tangu mapinduzi hayo yafanyike, serikali mpya ya kijeshi ya Niger imefungua mipaka na anga yake kwa nchi tano majirani zake.

Mipaka na Mali, Burkina Faso, Algeria, Libya na Chad imefunguliwa tena ingawa jeshi hilo limetangaza kwamba mipaka ya Niger na Benin na Nigeria itaendelea kufungwa kwa muda zaidi.

Jeshi hilo pia limeteua magavana wapya kwa majimbo manane yaliyoko nchini humo.

Ujerumani haiondoi majeshi yake Niger kwa sasa

Haya yanafanyika wakati ambapo mataifa ya Ulaya yako katika harakati za kuwaondoa raia wake nchini humo ingawa majeshi ya baadhi ya nchi hizo bado yanaendelea kusalia.

Niger Niamey Junta-Führer Amadou Abdramane
Kiongozi wa jeshi la Niger Kanali Meja Amadou AbdramanePicha: ORTN - Télé Sahel/AFP

Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Boris Pistorius amesema haoni haja ya kukiondoa kikosi cha wanajeshi 100 wa Ujerumani kilichoko Niger.

"Nilizungumza kwa simu na kamanda wa kambi yetu Niamey jana na aliniambia wazi kwamba hawana wasiwasi kuhusiana na usalama wao kwa sasa. Wana mawasiliano ya karibu na jeshi la Niger. Wanapata kila wanachokitaka kwa hiyo tunasubiri tuone hali itakavyokuwa kama wanavyosubiri wengine wengi," alisema Pistorius.

Haya ni mapinduzi ya saba ya kijeshi kutoka chini ya miaka mitatu katika kanda za Afrika Magharibi na Kati na yamezua mgawanyiko katika jumuiya ya ECOWAS.

Vyanzo: Reuters/ DPAE