Ujerumani yazindua mkakati mpya wa kulinda hali ya hewa
26 Aprili 2007Ujerumani leo imezindua mapendekezo ya kupunguza kiwango cha gesi ya carbon dioxide kutoka viwandani kwa silimia 40 katika kipindi cha miaka 13 na kuwa nchi iliyofanikiwa katika matumizi ya nishati duniani. Waziri wa mazingira wa Ujerumani, Sigmar Gabriel, ametoa mwito kiwango cha euro bilioni tatu kitolewe kugharamia uwekezaji katika kujenga teknolojia ya kupunguza matumizi ya nishati. Aidha waziri Gabriel amedokeza kuwa vibali vya kuruhusu viwanda kutoa gesi angani huenda vikaanza kuuzwa katika minada badala ya kutolewa bure kama ilivyo hivi sasa.
´Serikali ya Ujerumani inataka mwaka huu kuanzisha mpango mpya wa kuilinda hali ya hewa ambao kupitia uamuzi wa Umoja wa Ulaya utaanza kutekelezwa. Kupunguzwa kwa asilimia 40 kuna maana kupunguza tani milioni 270 za gesi za viwandani kupita kiwango kilichowekwa mwaka jana 2006. Matokeo ya mwanzo ya utafiti uliofanywa na serikali ya Ujerumani yamedhihirisha hilo linawezekana.´
Akizungumza bungeni mjini Berlin hii leo waziri Sigmar Gabriel, amesema Ujerumani ambayo inaongoza kiuchumi barani Ulaya, inahitaji kuboresha utendaji wake katika matumizi ya nishati kwa asilimia tatu kila mwaka ili kufikia kikwango kilichowekwa na Umoja wa Ulaya cha kupunguza gesi ya carbon dioxide kwa asilimia kati ya 20 na 30 kufikia mwaka wa 2020. Kiongozi huyo pia amesema anataka kuvihusisha viwanda katika kujaribu kulifikia lengo la Ujerumani kutaka kupunguza gesi ya carbon dioxide angani kwa asilimia 40.
Waziri Sigmar Gabriel amesema mkakati mpya wa kuilinda hali ya hewa unazingatia nafasi ya kiuchumi ya Ujerumani. Amesema Ujerumani ina nafasi nzuri katika siku za usoni kuchukua jukumu kubwa la kuongoza soko la nishati na inataka kuitumia nafasi hiyo.
´Hakujatokea wakati kama huu ambapo sera ya kuilinda hali ya hewa imekuwa muhimu kupunguza gharama kama wakati huu. Haijawahi kutokea kwamba jumuiya ya kimataifa imeamua na kuungana kufanya kazi kwa pamoja. Haijatokea pia kwa walimwengu kuwa tayari kushiriki katika juhudi za kulinda hali ya hewa. Ni kwa sababu wanaona watapata manufaa katika bajeti zao za matumizi, hali ya maisha na kwa kuwa wana wasiwasi kuhusu watoto wao pamoja na wajukuu wao.´
Kiongozi wa chama cha muungano cha CDUCSU bungeni, Katherin Reiche, amesema haitakuwa rahisi kwa mkakati mpya wa Ujerumani kufaulu bila kuzijumilsha Marekani, India na China. Hata hivyo ana matumaini kwamba mkutano wa mataifa yaliyoendelea zaidi kiviwanda ya G8 uliopangwa kufanyika mjini Heiligendamm, utakuwa ishara muhimu kwa mkutano wa Umoja wa Mataifa utakaozungumzia mabadiliko ya hali ya hewa mwezi Disemba mwaka huu nchini Bali.
´Ujerumani na Umoja wa Ulaya haziwezi kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa peke yao. tuna sehemu kati ya asilimia 15 ya gesi za viwandani duniano kote. Hata hivyo tunatakiwa kuchukua jukumu la kuongoza linapokuja swala la ulinzi wa hali ya hewa.´
Mpango aliouwasilisha waziri Gabriel leo unabashiri kupungua kwa matumizi ya umeme kwa asilimia 11 kufikia mwaka wa 2020. Kukarabatri vituo vya kutengeneza umeme kutumia teknolojia ya kisasa kutapunguza tani milioni 30 ya gesi ya carbon dioxide kufikia wakati huo. Waziri huyo ametoa mwito nishati ya jua na upepo itumiwe zaidi katika kutengeneza umeme na matumizi ya umeme yapuunguzwe.