Ujerumani yawasili Urusi tayari kwa kombe la dunia
12 Juni 2018Kikosi cha vijana chipukizi wa England kinachoongozwa na kocha Gareth Southgate pia kilitarajiwa kuwasili leo wakati shauku ikiongezeka kabla ya ufunguzi rasmi wa fainali hizo hapo Alhamis mjini Moscow kati ya wenyeji wa mashindano hayo Urusi dhidi ya saudi Arabia.
Lakini kabla ya shughuli hiyo kuanza uwanjani , wanachama wa shirikisho la kandanda duniani FIFA watakuwa na kibarua cha kuchagua iwapo wayazawadie mataifa ya Amerika ya kaskazini ama Morocco uenyeji wa michuano ya fainali za mwaka 2026.
Ujerumani , ambayo iliiangusha Argentina katika fainali nchini Brazil miaka minne iliyopita , inalenga kujiunga na Brazil kama washindi mara tano wa taji hilo lakini kuna maswali kuhusiana na jinsi wanavyocheza kwa sasa wakati wakiingia katika mashindano haya.
Kikosi cha Joachim Loew kimecheza michezo mitano bila ya kushinda kabla ya kufanyakazi ya ziada na kuishinda Saudi Arabia kwa mabao 2-1 katika mchezo wao wa mwisho wa kujiweka tayari na mlinda mlango namba moja Manuel Neuer haja cheza katika ligi tangu Septemba mwaka jana.
Wajerumani hufika angalau nusu fainali
Lakini Wajerumani wamefika angalau katika nusu fainali katika fainali nne za kombe la dunia na timu hiyo ina tabia ya kuanza kucheza vizuri wakati wanahitaji kufanya hivyo sana.
Mabingwa hao watetezi wanaaza kampeni yao ya kombe la dunia dhidi ya Mexico Juni 17 mjini Moscow. Pia wanacheza dhidi ya Sweden ba Korea kusini katika kundi F.
Ujerumani haiendi Urusi kutalii, "lakini kushinda mashindano hayo," amesema mkurugenzi wa timu hiyo Oliver Bierhoff.
England sio miongoni mwa timu zinazopigiwa upatu kutoroka na kombe hilo nchini Urusi lakini kikosi hicho cha tatu cha vijana chipukizi kinachokwenda na chapa ya Simba watatu kinaingia katika kinyang'anyiro hicho cha kombe la dunia kikijivunia nyota wa ligi ya England ya Premier League Harry Kane, Dele Alli na Raheem Sterling.
Tuna timu ya vijana wadogo lakini wenye uchu ambao wanataka kufika mbali , tunataka kuileta nchi yetu pamoja na kufanikisha kitu kikubwa," alisema Alli.
Wapinzani wa Uingereza katika kundi G Ubelgiji walionesha vipaji vyao katika ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Costa Rica mjini Brussels siku ya Jumatatu, ikiwa ni pamoja na mabao mawili kutoka kwa mshambuliaji wa Manchester United Romelu Lukaku na nyota wao Hazard kutoka Chelsea.
Hazard aliondoka uwanjani akichechemea mchezo ukiwa bado dakika 20 kumalizika lakini kocha Roberto Martinez alipuuzia wasi wasi huo , akisema hakuna sababu ya kuwa na wasi wasi kuhusu hilo.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Mohammed Abdul Rahman