Ujerumani yaukataa mpango wa "dhamana za euro"
3 Desemba 2011Akizungumza na wabunge hapo jana, Merkel alisema mataifa 17 yanayotumia sarafu ya euro yanapaswa kufanya kazi pamoja kuimarisha misingi ya umoja wao.
Merkel anapanga kukutana na Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa hapo Jumatatu kujadili mabadiliko katika Mkataba wa Umoja wa Ulaya kabla ya mkutano wa kilele wa viongozi wa Umoja huo, unaofanyika mwishoni mwa wiki ijayo. Katika hotuba aliyoitoa kwenye mji wa kusini mwa Ufaransa wa Toulon hapo juzi, Sarkozy alitoa msimamo sawa na wa Merkel, akisema kwamba Ulaya inapaswa kuundwa upya na kusisitiza nidhamu ya kifedha na mshikamano.
Wakati huo huo, Waziri wa Fedha wa Ujerumani, Wolfgang Schäuble, amerejelea msimamo wa serikali yake kukataa kile kinachoitwa "dhamana za euro". Katika mahojiano yake na gazeti la Passauer Neue Presse, Schäuble amesema uchumi wa Ujerumani utaelemewa sana, ikiwa serikali italazimika kuchukuwa dhamana za madeni, ya nchi zote za sarafu ya euro.
Wazo la kuanzisha "dhamana za euro" linaungwa mkono na baadhi ya serikali za mataifa yanayotumia sarafu hiyo, kama njia ya kupunguza gharama za kukopa kwa mataifa yenye matatizo ya kiuchumi. Ujerumani inahoji kwamba kuanzishwa kwa mpango huo, kutapunguza nguvu za kuwekwa kwa nidhamu ya kifedha.