Ujerumani yaukaribisha uamuzi wa rais Obama kuhudhuria mkutano wa copenhagen
6 Desemba 2009BERLIN
Ujerumani imeukaribisha uamuzi wa Rais Barack Obama kuhudhuria siku ya mwisho ya mkutano wa kimataifa wa hali ya hewa huko Copenhagen. Awali Obama alipangiwa kuhudhuria kikao cha tarehe 9, lakini sasa atakuwepo tarehe 18, wakati viongozi wengi wa dunia watakuwepo huko Copenhagen.Waziri wa mazingira wa Ujerumani, Norbert Roettgen aliliambia gazeti la BILD, uamuzi wa Obama ulikuwa ishara kamili, rais huyo wa Marekani alitaka ufanisi katika kupatikana kwa mpango wa kupunguza gesi zinazochafua mazingira. Afisa wa ngazi za juu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na mazingira, Achim Steiner alisema uamuzi wa Obama unaashiria kuwa maafikiano yanawezekana. Inatarajiwa mkutano wa Copenhagen utaafikia makubaliano mapya yatakayochukua mahali pa makubaliano ya Kyoto yanayomalizika muda wake 2012.