Ujerumani yatoa heshima za mwisho kwa Wolfgang Schäuble
22 Januari 2024Takriban watu 1,500 wamekusanyika kwenye hafla hiyo ya kumbukumbu ya Schäuble Wakiwemo viongozi wa kada mbali mbali za juu ikiwa ni pamoja na Rais wa Ufaransa Emmnuel Macron.
Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz, Rais wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier na spika wa bunge la Ujerumani Bärbel Bas ni miongoni mwa wale walioshiriki hafla hiyo.
Soma pia:Olaf Scholz asema Ujerumani imempoteza mwanasiasa mweye shauku
Schäuble, ambaye alinusurika jaribio la mauaji mnamo 1990, alihudumu katika bunge la Ujerumani chini ya chama cha kihafidhina cha Christian Democrats (CDU) kwa takriban miaka 51 kutoka 1972 hadi kifo chake mnamo Desemba 26 akiwa ndio mwanasiasa aliyelitumikia bunge kwa muda mrefu zaidi kupitia CDU.
Schäuble alishikilia nyadhifa mbali mbali za uwaziri. Pia aliongoza mazungumzo ya kuungana upya Ujerumani mbili, ya Mashariki na Magharibi mwaka 1990, akiwa waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Magharibi chini ya Kansela wa zamani Helmut Kohl.
Soma pia: Waziri wa zamani wa fedha wa Ujerumani afariki dunia
Lakini pia Shauble atakumbukwa kama mwanasiasa na kiongozi aliyesimama kidete kushinikiza hatua za kubana matumizi wakati wa mgogoro wa kiuchumi wa kanda ya inayotumia sarafau ya Yuro akiwa waziri wa fedha chini ya kansela wa zamani Angela Merkel.
Katika miaka yake ya mwisho,Schäuble alikua mwanachama wa kawaida wa chama hicho cha CDU. Alifariki dunia akiwa na umri wa 81 katika mji alikozaliwa wa Offenburg Kusini-Magharibi mwa Ujerumani, eneo aliloliwakilisha bungeni kwa zaidi ya nusu ya miaka yake na tayari ameshazikwa katika eneo hilo.