Kombe la Dunia la Wanawake: Ujerumani yatinga robo fainali
16 Juni 2015Ushindi huo uliiweka Ujerumani kileleni mwa kundi B. Melanie Leupolz na Lena Petermann waliwaweka Ujerumani kifua mbele kuelekea katika 16 za mwisho ambako huenda wakakutana na mojawapo ya timu imara zitakazomaliza katika nafasi ya tatu katika makundi yao. Petermann alifunga mabao mawili naye Sara Däbritz akaongeza la nne.
Norway ilipata ushindi wa mabao matatu kwa moja dhidi ya Cote d'Ivoire ili kufuzu katika robo fainali katika nafasi ya pili ya kundi hilo.
Kampeni ya Ujerumani inarejea tena Jumamosi Juni 20 mjini Ottawa ambako itashuka dimbani katika mchuano wa robo fainali.
Wenyeji Canada na China pia waliweza kujikatia tikiti zao za hatua ya mchujo baada ya kutoka sare katika mechi zao.
Canada walifungana 1-1 na Uholanzi na hivyo wakaongoza Kundi A mbele ya China waliopata sare ya 2-2 na New Zealand.
Timu hizo nne yaani Ujerumani, Norway, Canada na China zinajiunga na mabingwa Japan na Brazil katika robo fainali.
Katika mechi zijazo, Kundi F Mexico watakabana koo na Ufaransa wakati England wakiangushana na Colombia. Katika Kundi E Costa Rica watawaalika Brazil nao Korea Kusini wakivaana na Uhispania.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP
Mhariri: Abdulrahman