1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yatinga nusu fainali Euro ya wanawake

22 Julai 2022

Timu ya taifa ya Ujerumani ya kandanda la wanawake imetinga nusu fainali ya michuano ya Euro 2022 kwa wanawake baada ya kuibamiza Austria 2-0.

https://p.dw.com/p/4EUmv
UEFA-Frauen-EM 2022 Deutschland vs. Österreich
Picha: Dylan Martinez/REUTERS

Mtanange huo ulisadifu kuwa mgumu kwa Ujerumani lakini ulimalizika kwa kuiwezesha timu hiyo kusonga mbele katika kampeni yake ya kutwaa ubingwa wa kandanda la wanawake barani Ulaya kwa mara ya tisa.

Austria ilijitutumua wakati wa mchezo huo uliopigwa mjini London na wachezaji wake walikosakosa kuzitingisha nyavu za Ujerumani mara tatu.

Lakini yalikuwa ni magoli ya Lina Magull na Alexandra Popp ndiyo yaliiwezesha Ujerumani kuelekea nusu fainaili na kuifungasha virago Austria.

"Mchezo huo ungeweza kumalizika kwa bao 6-3" amesema kocha wa timu ya taifa ya wanawake ya Ujerumani Martina Voss-Tecklenburg akisema walicheza dhidi ya timu yenye uwezo mkubwa lakini bado anaamini timu anayoiongoza ilistahili kuondoka uwanjani kifua mbele.

Nusu fainali baada ya mshike mshike wa tangu hatua ya makundi 

UEFA-Frauen-EM 2022 Deutschland vs. Österreich
Kocha wa timu ya wanawake ya Ujerumani Martina Voss-Tecklenburg akifuatilia mchezo uliowapeleka nusu fainali.Picha: Alessandra Tarantino/AP Photo/picture alliance

Ujerumani inakwenda nusu fainali baada ya kupita kwenye tanuri la moto kutokea kwenye kundi linaloaminika kwamba lilikuwa gumu.

Ilijitengenezea njia ya kutinga hatua ya mtoano baada ya kuzishinda Denmark, Uhispania na Finland wakati wa hatua ya makundi.

Austria nayo tayari ilikwishaonesha makali kwenye hatua ya makundi pale ilipoilaza England bao 1-0 katika mechi ya kwanza kabisa ya ufunguzi wa michuano ya Euro kwa wanawake na kisha baadae iliirejesha nyumbani timu ya taifa ya Norway wakati wa hatua ya makundi.

Miaka mitano iliyopita timu ya wanawake ya Austria iliruka vihunzi na kufika hatua ya nusu fainali wakati michuano ya Euro mwaka 2017 ambayo kwa zama hizo ndiyo ilikuwa mashindano pekee makubwa kwa timu hiyo kuwahi kushiriki.

Na katika mchezo wa jana Alhamisi ilikuwa nusura wapate tena mafanikio hayo mnamo kipindi cha pili. Mshambuliaji wa Austria    Barbara Dunst  alipoteza nafasi kidogo tu za kutingisha nyavu za Ujerumani pale alipopiga shuti kali lililogonga nguzo za goli na kushindwa kuzaa matunda.

Sarah Puntigam naye pia aliwambisha mpira kwenye kingo za goli wakati wachezaji wa Ujerumani walipokuwa wakipambana kuondoa hatari golini kutoka mpira wa kona.

Nani kupambana na nani nusu fainali?

UEFA-Frauen-EM 2022 Deutschland vs. Österreich
Picha: Nigel Keene/Pro Sports Images/IMAGO

Baada ya mbinde zote hizo za Austria, Ujerumani ilirejesha utimamu uwanjani na huenda ingepata mabao mengi zaidi iwapo wachezaji wake wangechangamsha miguu. 

"Tulikuwa na bahati kidogo kwa sababu tuliwapa nafasi nyingi. Tunafuraha sana kwamba tumefikia hatua ya nusu fainali " amesema kiungo wa Ujerumani, Lina Magull, ambaye bao lake ni miongoni mwa mawili yaliyoiwezesha timu yao kusonga mbele.

Bao 2 ziliwatosha Ujerumani na sasa watasubiri matokeo ya mchezo kati ya Ufaransa na Uholanzi kufahamu watateremka dimbani na timu gani kukwaana siku ya Jumamosi kwenye mchezo wa nusu fainali.

England ilikwishatangulia nusu fainali tangu siku ya Jumatano na yenyewe itasubiri mchezo wa hii leo kati ya Sweden na Ubelgiji kujua itakwaana na nani kwenye mchezo wa nusu fainali.