1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yatangaza uwezo wa kudhibiti maambukizi ya corona

17 Aprili 2020

Ujerumani imesema mfumo wa huduma ya afya nchini humo, umefanikiwa kudhibiti mripuko wa virusi vya corona, wakati ambapo idadi ya wagonjwa waliopona ikiwa kubwa kuliko maambukizi mapya ya kila siku, kwa wiki hii.

https://p.dw.com/p/3b5NH
Deutschland Corona-Pandemie | PK Spahn
Picha: picture-alliance/AP Images/J. MacDougall

Hayo yameelezwa na Waziri wa Afya wa Ujerumani, Jens Spahn wakati akizungumza na waandishi habari mjini Berlin. Jens amesema mfumo wa afya wa Ujerumani haujawahi kuzidiwa na wagonjwa katika kipindi chochote kile. Ujerumani imeshika nafasi ya tano duniani kwa kuwa na visa vingi vya COVID-19 ikiwa nyuma ya Marekani, Uhispania, Italia na Ufaransa, huku ikiwa na wagonjwa 134,000 na vifo 3,868. Jens amesema ugonjwa huo sasa umeweza kudhibitiwa.

''Katika kukabiliana na janga la virusi vya corona, Ujerumani inafanya vizuri ukilinganisha kimataifa. Hali hii inatufanya tuwe wanyenyekevu, lakini sio kujiamini sana. Hadi sasa tumewapima zaidi ya watu milioni 1.7 virusi vya corona nchini Ujerumani. Idadi hiyo ni sawa na watu 350,000 kwa wiki. Tunafanya kazi kila siku na hali imeimarika,'' alibainisha Jens.

Siku ya Jumatano, Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel alisema nchi hiyo itaanza kuchukua hatua ndogo katika kufungua maduka kadhaa wiki ijayo na shule kuanza Mei 4. Wakati huo huo, jimbo la Saxony nchini Ujerumani limewaamuru wakaazi wake kuvaa barakoa wakati wakienda kufanya manunuzi au wanapotumia usafiri wa umma.

Coronavirus - Sachsen empfängt Hilfslieferung
Waziri Mkuu wa jimbo la Saxony, Michael KretschmerPicha: picture-alliance/dpa/Zentralbild/P. Endig

Waziri Mkuu wa jimbo hilo, Michael Kretschmer amesema leo kuwa raia hawatolazimika kuvaa barakoa za kitabibu, bali kitambaa tu au kitu sawa na hicho kinatosha kujifunika pua na mdomo. Saxony ni jimbo la kwanza kutangaza ulazima wa kufunika uso baada ya serikali ya shirikisho siku mbili zilizopita kupendekeza watu kuvaa barakoa. Amri hiyo itaanza kutekelezwa siku ya Jumatatu.

Ama kwa upande mwingine, Italia imetangaza mpango wake wa kuzindua programu maalum ya kufuatilia maambukizi ya virusi vya corona, wakati nchi hiyo ikijiandaa kuondoa masharti ya kuwataka watu kubakia majumbani na kusitisha huduma kadhaa, mapema mwezi Mei. Kamishna anayehusika na kusimamia janga la virusi vya corona, Domenico Arcuri jana alisaini amri hiyo, ambapo mkataba wa kuendesha programu hiyo umekabidhiwa kwa kampuni ya Bending Spoons ya mjini Milan.

Umoja wa Ulaya ulipendekeza kuwepo programu za kwenye simu ya mkononi za kisasa kama sehemu ya kufuatilia maambukizi ya virusi vya corona ili kuzisaidia nchi za umoja huo kulegeza masharti ambayo yamesababisha kushuka kwa uchumi katika umoja huo.

Wakati hayo yakijiri, serikali ya Austria imetangaza leo kuwa makumbusho na maktaba zitaruhusiwa kufunguliwa katikati ya mwezi Mei. Austria ilikuwa ni miongoni mwa nchi za kwanza za Umoja wa Ulaya kutangaza kuondoa hatua kwa hatua vizuizi vilivyowekwa katika kukabiliana na kusambaa kwa virusi vya corona. Maduka madogo, maeneo ya bustani na maduka ya DIY yalifunguliwa nchini humo tangu siku ya Jumanne.

Nchi jirani ya Slovenia imesema maduka madogo yataruhisiwa kufunguliwa kuanzia wiki ijayo, ikiwemo maduka ya vifaa, maduka ya vipuri vya magari na maeneo ya kufulia nguo, huku saluni na maduka ya urembo yakifunguliwa Mei 4.

 

(AFP, Reuters, DW https://bit.ly/2RM9iRS)