Ujerumani yatangaza mpango wa kufunga vinu vya nyuklia
30 Mei 2011Viongozi wa vyama vinavyounda serikali ya mseto, vya DCU/CSU na FDP, walikutana katika ofisi za Kansela Angela Merkel kujadili mpango huo wa kuvifunga vinu hivyo katika muda wa muongo mmoja, kutokana na hofu ya wanachi ya kuzuka mkasa kama ule wa Fukushima, Japan.
Waungaji mkono wa biashara ya nishati ya kinyukliya katika serikali ya mrengo wa kulia ya Merkel, walitaka hadhari ichukuliwe katika suala hilo, wakionya kuwa ukosefu wa umeme utadidimiza biashara.
Lakini hatimaye, baada ya majadiliano ya muda wa masaa 12 kati ya Kansela Merkel na viongozi wa vyama hivyo vitatu, makubaliano yalifikiwa.
Serikali iliafiki kuweka akiba ya nishati kiwango cha megawati 2000, ambacho ni kiwango sawa na vinu viwili vya nyuklia vitakavyotumika wakati wa dharura, fikra ambayo wataalamu wanaitazama kuwa vigumu kutekeleza.
Waliokuwemo pia katika majadiliano hayo ni wakuu wa vyama viwili vikuu vya upinzani, Social Democrats, na chama cha kijani. Kansela Merkel amesema anatarajia kuchora sera ya pamoja ili kumaliza mzozo huo ulioigawanya Ujerumani tangu miaka ya 1970.
Jopo la mapadri, wasomi, na viongozi wengine wa kijamii ,idadi jumla watu 17, siku ya Jumamosi walimpendekeza kwa kansela Merkel kuwa Ujerumani isitishe matumizi ya nyuklia katika muda wa mwongo mmoja kutoka sasa, kwa kuvifunga vinu vinane hivi sasa na vyengine 9 taratibu.
Utafiti wa kina wa jopo hilo unatarajiwa kutangazwa rasmi hii leo kwa umma, ukiwemo mpango wa kujenga vinu vya gesi na utumiaji wa nishati ya upepo, kutoa asilimia 22 ya umeme unaotumika hivi sasa Ujerumani kutokana na nishati ya nyuklia.
Sheria iliyopitishwa mwaka uliopita inaitaka Ujerumani kuvifunga vinu vyake hivyo ifikapo mwaka 2036. Utafiti wa maoni unaonyesha kuwa idadi kubwa ya Wajerumani wanataka vinu hivyo vifungwe mapema mno, baada ya kutokea tetemeko la ardhi la tarehe 11 Machi na tsunami huko kaskazini mashariki mwa Japan. Maafa hayo yaliviharibu vinu vya nyuklia vya Fukushima Daiichi na kusabaisha kuvuja kwa miale ya sumu.
Uamuzi huo bado unahitaji kufikishwa bungeni na kuwepo viongozi wa upinzani wa chama cha Social Democrats na kile cha Kijani, katika mazungumzo hayo kumesaidia kufikiwa makubaliano yanayoungwa mkono na watu wengi..
Hatahivyo, huenda uamuzi huo ukakabiliwa na upinzani kutoka kwa kampuni za RWE, E.ON, Vattenfall na EnBW, kampuni zinazotengeneza umeme na zinazovisimamia vinu hivyo 17, zaidi kutokana na mipango ya kuendeleza kodi ya nishati hiyo ya nyuklia.
Duru zinaarifu kuwa serikali inafikiria kuondoa kodi hiyo ili kampuni hizo nne kuu ziunge mkono kusitishwa nishati hiyo ya nyuklia, na isiishtaki serikali kwa kuigeuza sera yake.
Mwandishi: Maryam Abdalla/DPAE/Reuters
Mhariri: Othman Miraji