Ujerumani yatambua wajibu wake kwa Vuguvugu la Warsaw
1 Agosti 2019Katika hafla ya kumbukumbu hiyo mjini Warsaw, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Heiko Maas alisema kuwa serikali ya Ujerumani na watu wake wanaona aibu sana kutokana na kile kilichotendwa na wanajeshi wa Kijerumani ndani ya ardhi ya Poland, na inabeba jukumu lake la kimaadili kwayo.
Lakini kwenye suala tata ambalo mara kwa mara limerejelewa na wanasiasa wa Poland kudai fidia kwa uovu wa Wanazi, Waziri Maas alisema hilo ni jambo lisilowezekana kwa upande wa Ujerumani.
"Kuhusiana na fidia, kutokana na mtazamo wa kisheria, jambo hilo kwa Ujerumani limekwisha, lakini kumbukumbu na marekebisho kamwe hayawezi kwisha kwa Ujerumani. Ujerumani inahisi kuwa na jukumu kwenye Vita vya Pili vya Dunia na kile ambacho imeitendea Poland," alisema Waziri Maas mbele ya waandishi wa habari.
Hata hivyo, akizungumza kwenye mkutano huo huo na waandishi wa habari akiwa na Maas, Waziri wa Mambo ya Nje wa Poland, Czaputowicz, alitilia mkazo kwamba ndani ya nchi yake kuna hisia za kutotendewa haki ama ukosefu wa fidia kwa madhara yaliyotendeka wakati wa Vita vya Pili vya Dunia.
Fidia ya euro bilioni 41
Kwa mujibu wa waziri huyo wa mambo ya nje wa Poland, bunge la nchi yake limeteuwa kamati maalum ya kutathmini kiwango cha madhara hayo.
Mnamo mwaka 2004, meya wa wakati huo wa mji mkuu wa Warsaw na rais wa baadaye wa Poland, Lech Kaczynski, alisema gharama za madhara ya Wajerumani kwenye mji wake zilikuwa sawa na euro bilioni 41.
Waziri wa mambo ya nje wa Poland amesema kuwa tathmini ya bunge itakuwa sehemu ya majadiliano katika siku zijazo.
Vuguvugu la Warsaw limeendelea hadi sasa kufunika mahusiano baina ya mataifa haya mawili jirani. Hata hivyo, kuhudhuria kwa Maas kwenye kumbukumbu hizo za miaka 75, ikiwa ni mara ya kwanza kwa kiongozi wa ngazi za juu tangu pale Kansela Gerhard Schröder alipofanya hivyo mwaka 2004, kunatajwa kufunguwa ukurasa mpya.
Vuguvugu la Warsaw
Tarehe 1 Agosti mwaka 1944, watu 200,000 - wengi wao wakiwa raia - waliuawa au kunyongwa baada ya jaribio la kuutwaa mji mkuu wa Poland, Warsaw, kutoka mikononi mwa Wanazi. Maelfu ya wengine walipelekwa kwenye makambi ya mateso.
Wapiganiaji ukombozi walikuwa wakitarajia kupata msaada kutoka nje, lakini vifaa vilivyodondoshwa na ndege za majeshi ya Washirika zilikuwa zikikosea mahala pa kuangusha, na licha ya vikosi vya Kisovieti kuwapo karibu, serikali mjini Moscow ilikataa kuwasaidia wapiganaji hao kutokana na uhusiano wao na serikali inayopingana na ukomunisti na ambayo ilikuwa ikiishi uhamishoni.
Wapiganaji hao walifanikiwa kupambana kwa siku 63 kabla ya kushindwa tarehe 2 Oktoba 1944. Muda mfupi baadaye, kiongozi wa Kinazi Adolf Hitler aliamuru kuharibiwa kabisa kwa mji wa Warsaw, ambapo asilimia 90 ya majumba ya kihistoria yaliripuliwa, ikiwemo kasri ya kifalme.
Idadi ya wakaazi wa mji huo ilikaribia watu milioni moja wakati vuguvugu linaanza, lakini wakati linamalizika walibakiwa watu elfu kadhaa tu waliokuwa wakiishi kwenye vifusi vya mji ulioangamizwa.