Ujerumani yasubiri matokeo ya uchaguzi
26 Septemba 2021Wagombea watatu wakuu wa Ukansela wote wamepiga kura mapema kabisa hii leo ambapo Olaf Scholz alipiga kura huko Berlin. Mgombea wa muungano wa vyama ndugu CDU/CSU Armin Laschet nae pia alipiga kura yake mjini Aachen na kisha kuwatolea mwito wajerumani wajitokeze kwa wingi kupiga kura.
"Sote tunahisi huu ni uchaguzi muhimu kabisa,uchaguzi utakaoamua Ujerumani itachukua mwelekeo gani katika miaka inayokuja kwahivo kila kura ina umuhimu. Na ndio sababu natumai kwamba kila mmoja atatumia haki yake ya kupiga kura ili mwishowe serikali ijayo iundwe kidemokrasia'' alisema Laschet.
Kura ya Laschet yaibua kadhia
Hata hivyo Armin Laschet anakabiliwa na kadhia kubwa baada ya kukiuka sheria ya uchaguzi ya kutakiwa kuweka siri chama alichokipigia kura kwa kuionesha waziwazi karatasi yake ya kupiga kura kabla ya kuitumbukiza kwenye boksi la kura. Laschet aliifunua karatasi yake ya kura na kuionesha kwa waandishi habari kwa ajili ya kupiga picha kabla ya kuitumbukiza kwenye sanduku la kura.
Hata hivyo mkuu wa tume ya uchaguzi amesema kura ya Laschet haiwezi kubatilishwa kwasababu amekipigia chama chake mwenyewe kama alivyotarajiwa.Ingawa kosa hilo la bwana Laschet limeibuka miito ya kutaka kura yake ifutwe huku magazeti ya humu nchini tayari yakiwa yameshandika habari za kumkejeli sambamba na kwenye mitandao ya kijamii . Ama mgombea wa chama cha Kijani Annalena Baerböck baada ya kupiga kura yake alikuwa na haya ya kusema.
Soma pia:Wajerumani wapiga kura
''Jiamulie mwenyewe kwa uhuru''
''Ni ushindi wa demokrasia yetu ambayo inaamuliwa katika siku kama hii ya hali ya hewa ya jua,jiamulie mwenyewe kwa uhuru na kuiimarisha demokrasia. Kila kura inaumuhimu katika uchaguzi huu.Tumeona katika wiki za hivi karibuni ni kwa namna gani kinyang'anyiro hiki kitakavyokuwa.Tunataraji kwa kutazama kura za maoni,kwa kura nyingine kidogo zaidi tunaweza kwahakika kuwa na mwanzo mpya wa nchi hii'',alisema Baerbock.
Soma pia:Ni kina nani wagombea watatu wa Ukansela Ujerumani ?
Wakati huohuo imeripotiwa kwamba bomu la tangu wakati wa vita vya pili vya dunia ambalo halijaripuka limegunduliwa katika mji wa Wuppertal magharibi mwa Ujerumani na kutatiza shughuli ya upigaji kura. Wakaazi wa mji huo wametakiwa kutofika kwenye vituo vya kupiga kura vitano ambavyo viko karibu na eneo lilikogunduliwa bomu hilo.
Vituo vya Kupiga kura msikilizaji vitafungwa muda mchache ujao na bila shaka utaanza mchakato wa kura kuhesababiwa na kutangazwa kuanzia muda huo huo wa jioni hii. Mshindi bila shaka atajulikana sio masaa mengi kutoka sasa.