Ujerumani yasisitiza taifa la Israel kuwa na haki ya kuwapo
26 Aprili 2018"Haki ya Israel kuwapo na usalama wake ni mambo ambayo hayawezi kujadiliwa nasi," hoja iliyopitishwa kwa idadi kubwa ya wabunge wa bunge la Ujerumani imesema hii leo.
Mswada huo pia umeshutumu ongezeko la uhalifu unaofanywa kutokana na chuki dhidi ya Wayahudi nchini Ujerumani. "Haiwezekani kwamba idadi ya mashambulio inaendelea kuongezeka na kwamba Wayahudi nchini Ujerumani wanajihisi kuwa katika hatari," umeeleza muswada huo.
Hoja hiyo iliidhinishwa na wabunge kutoka katika vyama ndungu vya kihafidhina vinavyoongozwa na kansela Angela Merkel , washirika wao katika serikali ya mseto nchini Ujerumani chama cha Social Democratic Union, SPD , chama cha kijani, Free Democrats FDP pamoja na chama mbadala kwa Ujerumani AfD.
Chama cha siasa kali za mrengo wa kushoto cha Die Linke kilijiondoa kupiga kura wakati hoja ya ziada ambayo wanachama wake waliuandika pamoja na chama cha Kijani ilikataliwa. Chama cha Die Linke hakikujumuishwa katika kuandika hoja hiyo ya serikali ambayo hatimaye ilipitishwa.
Kulikuwa na hali ya kutupiana maneno wakati wa mjadala wakati kiongozi wa kundi la wabunge wa chama cha Kijani Katrin Goering-Eckardt alipokataa msimamo wa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha AfD kwamba chuki dhidi ya wayahudi sio kitu cha kweli; pia alimueleza kiongozi wa kundi la wabunge wa chama hicho Alexander gauland kuwa ni "chui aliyevaa ngozi ya kondoo."
Vyama vyalumbana
Kiongozi wa kundi la wabunge wa chama cha FDP Alexander Graf Lambsdorff aliwashutumu baadhi ya wanachama wa chama cha Die Linke kwa kuunga mkono kampeni ya vuguvugu ambalo liliisusia Israel pamoja na biadhaa za Israel likijulikana kama Susia, kutoweka vitega uchumi na vikwazo BDS.
Mbunge wa chama cha AfD Beatrix von Storch ameishutumu serikali ya Ujerumani kwa kuchochea kile alichosema kuwa ni chuki dhidi ya Israel katika mashariki ya kati kwa kuchangia fedha katika shirika la Umoja wa Mataifa linalotoa misaada na kazi kwa wakimbizi wa Palestina , UNRWA.
Hapo jana Wajerumani wa dini mbali mbali walivaa kofi za vibandiko vinavyovaliwa na wayahudi na kuingia mitaani katika maandamano yaliyofanyika katika miji mbali mbali wakipinga shambulio la chuki dhidi ya Wayahudi na kuelezea hofu yao juu ya kuongezeka kwa chuki dhidi ya Wayahudi nchini Ujerumani.
Maandamano hayo ya Kippa , kibandiko yalizuka kutokana na shambulio la mchana kweupe wiki iliyopita lililofanywa dhidi ya vijana wawili waliovalia kofia hizo za vibandiko katika kitongoji maarufu katika mji mkuu wa Ujerumani , Berlin.
Mwandishi: Sekione Kitojo / dpae / ape
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman