1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani:Hatua za kupambana na virusi vya corona zarefushwa

Daniel Gakuba
6 Januari 2021

Ujerumani imerefusha muda wa hatua kali za kupambana na kusambaa kwa virusi vya corona hadi tarehe 31 Januari. Uamuzi huo umefikiwa baada ya mkutano kati ya Kansela Angela Merkel na viongozi wa majimbo ya shirikisho.

https://p.dw.com/p/3nYNi
Berlin I Angela Merkel verkündet Verlängerung des Lockdowns
Hatua kali za kupamba na maambukizi ya corona zitaendelea hadi angalau mwishoni mwa JanuariPicha: Michel Kappeler/REUTERS

Akitangaza hatua hizo Jumanne usiku Kansela Angela Merkel amesema vikwazo vikali zaidi vitawekwa kuzuia watu kutangamana ili kudhibiti ongezeko la maambukizi.

Masharti yatakayotekelezwa nchini kote Ujerumani ni pamoja na kuendelea kuzifunga shule, hali kadhalika biashara na huduma zote zisizo za lazima hadi mwishoni mwa mwezi huu wa Januari. Masharti hayo ambayo yaliwekwa katikati mwa mwezi uliopita wa Desemba yalitarajiwa kumalizika tarehe 10 Januari.

Soma zaidi: Janga la Virusi vya Corona bado kuzungumkuti

Kansela Merkel amesema aina mpya ya virusi vilivyotoka nchini Uingereza, na msimu wa baridi vinaleta changamoto inayohitaji hatua kali za kukabiliana navyo.

''Nimesema mara kwa mara kwamba miezi ya msimu wa baridi, kama walivyotueleza wataalamu jana, ni wakati ambapo athari za janga hili zinaongezeka,'' amesema Kansela Merkel, na kuongeza kuwa kuwepo ''kirusi kilichojibadilisha ambacho tayari kimeonekana nchini humu, inatulazimu kuchukua hatua kali za tahadhari.''

Symbolbild I Verlängerung des Lockdowns in Deutschland
Mitaa mitupu katika mji wa Frankfurt kutokana na kufungwa kwa biashara zisizo za mahitaji ya lazimaPicha: Thomas Lohnes/Getty Images

Ongezeko kubwa la maambukizi na vifo

Tangu kuibuka kwa virusi vya corona, Ujerumani imekwishasajili visa milioni 1.8 vya maambukizi, na vifo 36,000 kutokana na virusi hivyo, hiyo ikiwa ni kwa mujibu wa takwimu za Chuo Kikuu cha Johns Hopkins.

Hatua mpya zilizotangazwa zinawataka wakazi katika katika maeneo yenye idadi kubwa ya maambukizi kutosafiri umbali wa zaidi ya km 15 kutoka nyumbani kwao bila sababu inayoeleweka.

Soma zaidi: Chanjo zaanza kutolewa katika Umoja wa Ulaya

Kila wilaya moja kati ya sita nchini Ujerumani inakidhi viwango vya kuwa eneo la maambukizi makubwa, ambayo kipimo chake ni maambukizi 200 kwa kila wakazi laki moja kwa muda wa juma moja.

Großbritannien Oxford | Coronavirus | AstraZeneca Impfstoff
Watu wa makundi maalumu yenye udhaifu ndio watapewa kipaumbele katika kupata dozi za kwanza za chanjoPicha: Steve Parsons/empics/picture alliance

Mikutano ya hadhara itaendelea kuzuiliwa, na kila familia itaruhusiwa kutembelewa na mtu mmoja tu kutoka nje.

Waajiri wamehimizwa kuwarahisishia watumishi wao kufanyia kazi nyumbani, na kuwapa likizo yenye malipo ya angalau siku kumi, wazazi wenye watoto wachanga ambao hawawezi kuwapeleka katika vituo vya kuwatunza wakiwa kazini.

Chanjo kwa wenye mahitaji zaidi kwanza

Aidha, Bi Merkel amesema anaamini watu wa makundi yanayokabiliwa na hatari zaidi ndio wataweza kupata chanjo mnamo robo ya kwanza ya mwaka 2021, akiongeza kuwa dozi za kutosha kuwachanja watu wengine wengi yumkini zitapatikana mnamo robo ya pili ya mwaka huu.

Soma zaidi: Marufuku ya safari dhidi ya Uingereza yaanza kuondolewa 

Kiongozi huyo amesema mkutano mwingine wa tathmini utafanyika tarehe 25 Januari.

Nchini Uingereza nako, serikali imesema masharti mapya ya kupambana na virusi vya corona huenda yakaendelea kuwepo hadi mwezi Machi, baada ya waziri mkuu Boris Johnson kusema usiku wa kuamkia leo kuwa moja kati ya wakaazi 50 wa Uingereza amepatwa na maambukizi ya corona.

Amesema matumaini ya kulishinda janga hilo yanawekwa katika operesheni ya chanjo, akiarifu kuwa tayari watu milioni 1.3 wamekwishapatiwa chanjo dhidi ya virusi hivyo hatari.

 

ape, afpe, https://p.dw.com/p/3nX98