1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yarefusha agizo la watu kutokaribiana

Babu Abdalla30 Aprili 2020

Kiongozi wa wafanyakazi katika ofisi ya Kansela amesema agizo la watu kutokaribiana limerefurushwa hadi Mei 10 wakati Ujerumani inafikiria kuangazia vikwazo ilivyoweka ili kukabiliana na maambukizi ya virusi vya Corona.

https://p.dw.com/p/3bchN
Deutschland Berlin Pressekonferenz  Coronavirus | Angela Merkel
Picha: Getty Images/AFP/K. Nietfeld

Katika mkutano unaotarajiwa kufanyika 30.04.2020 ili kuangazia vikwazo vilivyowekwa katika kukabiliana na kuenea kwa virusi vya Corona, Helge Braun amesema kuwa Kansela Angela Merkel pamoja na viongozi wengine watajadili kuhusu mipango ya kufungua shule na kurejelewa kwa halfa mbalimbali za michezo.

Hata hivyo watasubiri hadi Mei 6 watakapopata takwimu zaidi kuhusu athari za kuruhusu shughuli za kiuchumi kuendelea kabla ya kufanya uamuzi.

Wakati hayo yanaarifiwa, zaidi ya watu 300,000 wamepoteza kazi zao hapa Ujerumani katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita kutokana na athari za kiuchumi zilizosababishwa na janga la virusi vya Corona.

Waziri anayehusika na ajira na masilahi ya wafanyakazi, Hubertus Hei, amesema kuwa Ujerumani inakabiliwa na changamoto ya kihistoria.

Wakati huo huo, kitengo cha ligi kinachopanga ratiba za mechi za Bundesliga DFL, kimeanza leo Alhamisi kupima wachezaji ili kubaini iwapo wameambukizwa virusi vya Corona katika hatua ambayo inafungua uwezekano wa kurudi tena kwa mechi za ligi kuu ya kandanda ya Bundesliga kuanzia wiki ijayo.

Kiongozi wa wafanyakazi katika ofisi ya Kansela wa Ujerumani amesema hatma ya iwapo ligi ya Bundesliga itaanza tena huenda ikajadiliwa katika mkutano wa baadaye hii leo kati ya Angela Merkel na mawaziri wakuu wa majimbo 16 hapa Ujerumani.

Iran yatangaza vifo vipya 71 vinavyotokana na Covid-19

Iran Coronavirus Präsident Hassan Rohani
Rais Hassan Rouhani wa IranPicha: picture-alliance/AA/Handout Iranian Presidency

Na nchini Iran, wizara ya afya imetangaza vifo vipya 71 hii leo kutokana na ugonjwa wa Covid-19 na kupelekea idadi ya vifo vinavyotokana na homa hiyo ya mapafu kupindukia 6,000.

Msemaji katika wizara hiyo Kianoush Jahanpur amesema kuwa watu wengine 983 wamekutikana na virusi vya Corona na kufikisha idadi jumla ya watu walioambukiwa virusi hivyo kuwa 94,640.

Hata hivyo, idadi hiyo imetiliwa shaka na wataalamu na maafisa kutoka ndani na nje ya Iran.

Vile vile waziri wa afya ameonya kuwa Iran inatakiwa kujiandaa kwa mlipuko mwengine wa ugonjwa wa COVID-19 katika misimu ya vuli na baridi inayokuja.