1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yaongoza Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa

Oumilkheir Hamidou
2 Aprili 2019

Zamu ya Ujerumani kama mwenyekiti wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, Uchaguzi wa mabaraza ya miji nchini Uturuki na juhudi za kuwahimiza watu wachangie viungo vya mwili ni miongoni mwa mada magazetini .

https://p.dw.com/p/3G4Qo
USA New York | Deutschland übernimmt Vorsitz im UN-Sicherheitsrat | Heiko Maas, Außenminister
Picha: picture-alliance/dpa/R. Hirschberger

Tunaanzia New-York ambako tangu jana April mosi na kwa muda wa mwezi mmoja Ujerumani imekabidhiwa zamu ya mwenyekiti la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Gazeti la "Rhein-Zeitung" la mjini Koblenz linamulika malengo yanayotangulizwa mbele na Ujerumani katika taasisi hiyo muhimu zaidi ya Umoja wa Mataifa. Gazeti linaandika:

Mbali na juhudi za Umoja wa Mataifa za kulinda amani, serikali kuu ya Ujerumani inatanguliza mbele zaidi juhudi za kuepusha kutokea mizozo.

Mizozo isiachiwe hata kidogo kujiri. Na kule ambako mizozo inachomoza, Ujerumani inapanga kushajiisha mchango wa wanawake, kuwalinda wahudumu wa misaada ya kiutu na sera ya kukabailiana na mabadiliko ya tabianchi kama sehemu ya sera jumla ya usalama. Ujerumani na Ufaransa wanapigania muongozo wa kimataifa unaozingatia maoni ya mataifa tofauti dhidi ya maamuzi ya upande mmoja ya rais wa Marekani Donald Trump. Muongozo huo ndio unaotakiwa uwe dira na mfumo wa ushirikiano kwaajili ya ulimwengu wa amani."

Erdogan na chama chake wapoteza viti Istanbul na Ankara

Uchaguzi wa mabaraza ya mjini umemalizika nchini Uturuki, chama tawala cha AKP cha rais Recep Tayyip Erdogan kimeshindwa katika miji miwili mikubwa ya nchi hiyo; mji mkuu Ankara na mji mkuu wa kiuchumi Istanbul. Wahariri wanajiuliza kama huo ndio mwazo wa mwisho wa enzi za rais Erdogan. Gazeti la mjini Cologne, Stadt Anzeiger linaandika:"Baada ya chaguzi hizo Uturuki itavuta pumzi kidogo. Zoezi jengine la kupiga kura halitarajiwi kabla ya mwaka 2023. Erdgan ana muda wa miaka minne kwa hivyo kusawazisha mivutano ya ndani ya kisiasa na kuwanyooshea mkono wanaomkosoa. Anaweza kuanzisha mageuzi kadhaa ya kiuchumi ambayo kutokana na sababu za kimkakati za uchaguzi amekuwa miaka ya nyuma daima akiyaakhirisha. Na anaweza pia kusawazisha uhusiano uliodhoofika wa nchi za nje na hasa kuelekea Umoja wa Ulaya."

Viungo vya mwili kunusuru maisha

Mjadala umehanikiza nchini Ujerumani kuhusu umuhimu wa watu ambao wanaiaga dunia kuchangia viungo vya mwili ili kuokoa maisha ya wengine. Mapendekezo yanatolewa eti kama mtu hajausia viungo vyake vifanywe nini, basi serikali iwe na haki ya kuvitumia viungo hivyo kuwahui wengine wanaovitegemea  ili waaweze kuendelea kuishi. Maoni yanatafautiana sana katika mada hiyo tete. Gazeti la "Westfälische Nachrichten" linaandika:"Uamuzi wa mtu kuchangia viungo vya mwili ni uamuzi wa kibinafsi. Hakuna si mwanasiasa, si chama na wala si serikali inayopaswa kumshawishi mtu hata kama ni kwa maslahi ya ubinaadam.

Kwasababu katika  kuchangia viungo vya mwili, suala hapo halihusu pekee mwili wa binaadam, bali ni suala la mbingu na ardhi na ambalo bado halijapatiwa jibu lolote la kisayansi. Kwa uamuzi kama huo, panahitajika wazo la kina. Katika baadhi ya kadhia, wenye kuchangia viungo vyao vya mwili  hawaulizwi kqbisa kama wanataka au la ."

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse