1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yakataa asilimia 10 ya wakimbizi

24 Januari 2016

Wakati Ujerumani ikiwa bado inaendelea kupokea wahamiaji 2,000 kwa siku hivi sasa inawanyima vibali vya kuingia nchini wengine 200 kwa kupitia mipaka yake.

https://p.dw.com/p/1HjBR
Waziri wa Mambo ya ndani wa Ujerumani Thomas de Maizière
Waziri wa Mambo ya ndani wa Ujerumani Thomas de Maizière.Picha: Imago

Hatua kali za kudhibiti mipaka zimechukuliwa baada ya taifa hilo lenye nguvu kubwa za kiuchumi barani Ulaya mwaka jana kupokea wahamiaji na wakimbizi milioni 1.1 idadi iliovunja rekodi na iliohitaji rasilmali kubwa jambo ambalo limechochea mjadala mkali wa kisiasa.

Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Thomas de Maiziere ameliambia gazeti la Jumapili la "Bild am Sonntag" kwamba "watu wanaokimbia vita na ukandamizaji wanapatiwa ulinzi na hifadhi nchini Ujerumani. "Ameongeza kufafanuwa kwamba "lakini wale ambao hawahitajii ulinzi huo wanakataliwa mpakani kuingia nchini."

Amesema mtu yoyote yule ambaye hataki kuomba hifadhi ya kisiasa nchini Ujerumani na anataka kuingia nchini kinyume na sheria hana haki ya kubakia hapa.

Kwa mujibu wa waziri huyo hadi sasa polisi ya Ujerumani imewakatalia watu 200 kwa siku kuingia nchini kwa kulinganisha na watu 400 ambao walikataliwa kwa mwezi mzima wa Oktoba wakati udhibiti wa mipaka na taratibu za kujiandikisha zilipoelemewa na wimbi kubwa la wahamiaji na wakimbizi.Miongoni mwa waliorudishwa ni wale wanaotaka kuomba hifadhi katika nchi nyengine za Ulaya.

Wakimbizi 2,000 wanawasili kila siku

Wizara ya mambo ya ndani ya Ujerumani imesema hadi sasa licha ya kuwa ni kipindi cha baridi takriban wakimmbizi 2,000 wamekuwa wakiwasili kila siku. Polisi hivi sasa ina uwezo wa kuwasajili wakimbizi 3,500 kwa siku kwenye mipaka yake.

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani analaumiwa kwa sera yake ya milango wazi kwa wakimbizi.
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani analaumiwa kwa sera yake ya milango wazi kwa wakimbizi.Picha: picture-alliance/dpa/S. Hoppe

Kiongozi mwandamizi katika chama cha kihafidhina cha Kansela Angela Merkel amependekeza kuanzishwa kwa " vituo vya mpakani" kwenye mpaka na Austria ili kuharakisha kurudishwa makwao kwa watafuta hifadhi ambao hawastahiki kubakia nchini.

Julia Kloeckner kiongozi wa chama cha Merkel cha Christian Demokrat katika jimbo la magharibi la Rhineland- Palantinate alikuwa muangalifu kuutaja mpango huo kama " "Plan A2" badala ya "Plan B" akiongeza kusema kwamba hatua ya Merkel kushinikiza kuwepo kwa ufumbuzi wa Umoja Ulaya kukabiliana na wimbi kubwa la watu wanaotafuta hifadhi barani Ulaya bado lilikuwa sahihi.

Vituo vya mpakani

Katika waraka ambao ametowa msimamo wake huo amesema "wanataka kusaidia shinikizo hilo.Katika waraka huo Kloackner amependekeza kuanzishwe vituo vya mpakani kwenye mpaka na Austria.

Wakimbizi wakiwa katika ardhi ya Ulaya.
Wakimbizi wakiwa katika ardhi ya Ulaya.Picha: picture-alliance/dpa/C.Poppe

Pendekezo hilo ambalo limeidhinishwa na Katibu Mkuu wa Chama cha CDU linaonyesha hali ya kukataa tamaa ilioko kwenye chama hicho cha Merkel kutokana na kuzorota kupigwa kwa hatua katika kufanikisha ufumbuzi wa Ulaya nzima katika kukabiliana na mzozo wa wakimbizi ambao unaelemea miundo mbinu ya serikali nyingi za mitaa nchini Ujerumani.

Ujerumani mwaka jana ilipokea watafuta hifadhi milioni 1.1 na kupelekea kuzusha wito kutoka ullimwengu mzima wa kisiasa wa kutaka kufanyika mabadliko kwa jinsi inavyoshughulikia idadi ya wakimbizi wanaokuja Ulaya wakikimbia vita na umaskini nchini Syria,Afghanistan na kwengineko.

Wasi wasi unaongezeka wa Ujerumani unahusu uwezo wa nchi hiyo kukabiliana na wimbi hilo la wakimbizi na wasi wasi kutokana na uhalifu na usalama baada ya kushambuliwa kwa wanawake wakati wa mkesha wa mwaka mpya mjini Cologne.

Kuungwa mkono kwa chama cha Merkel CDU na chama ndugu CSU kumeshuka kwa asilimia mbili na kuwa asilimia 36 kwa kulinganisha na wiki iliopita.

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters/AFP

Mhariri : Yusra Buwayhid