1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yakaribisha kauli ya Putin kuhusu Ukraine

Josephat Nyiro Charo8 Mei 2014

Waziri wa mambo ya nchi za kigeni wa Ujerumani, Frank Walter Steinmeier, anasema kauli ya kutia moyo ya rais wa Urusi, Vladimir Putin, huenda ikasaidia juhudi za kutafuta suluhisho la kidiplomasia kwa mzozo wa Ukraine.

https://p.dw.com/p/1BvaX
Frank-Walter Steinmeier Bern
Picha: Reuters

Waziri wa mambo ya nchi za kigeni wa Ujerumani, Frank Walter Steinmeier, anasema kauli ya kutia moyo ya rais wa Urusi, Vladimir Putin, kutaka kura ya maoni mashariki mwa Ukraine icheleweshwe, huenda ikazipiga jeki juhudi za kutafuta suluhisho la kidiplomasia katika mzozo wa Ukraine.

Steinmeier amesema mapema leo "tumefikia wakati muhimu wa kupitisha maamuzi kufuatia mkutano kati ya Putin na rais wa Uswisi, Didier Burkhalter, ambaye nchi yake ni mwenyekiti wa Shirika la Usalama na Ushirikiano barani Ulaya, OSCE.

Putin alilegeza msimamo wake jana akitangaza kwamba Urusi imeviondoa vikosi vyake kutoka eneo la mpakani na Ukraine na kutaka kura ya maoni ya Jumapili ijayo mashariki mwa Ukraine iahirishwe. "Kwa hiyo tunawaomba wajumbe wa kusini mashariki mwa Ukraine na wafausi wanaounga mkono utawala wa shirikisho wa nchi hiyo waahirishe kura ya maoni iliyopangwa kufanyika Mei 11."

Hata hivyo Marekani na jumuiya ya kujihami ya NATO zinasema hakujajitokeza dalili zozote kuonyesha mambo hayo mawili yameanza kutekelezwa.

Waziri Steinmeier anasema kilichojadiliwa na Burkhalter "kinapaswa kutekelezwa mara moja." Steinmeier aidha anasema "bado kuna fursa ya kufaulu kupitia njia za kidiplomasia kuepusha ongezeko la machafuko."

Waasi watafakari pendekezo la Putin

Hii leo waasi wanaoiunga mkono Urusi mashariki mwa Ukraine wanatafakari kama waiahirishe kura ya maoni kutaka uhuru wao kutoka kwa Ukraine, kufuatia kauli ya rais Putin iliyopunguza makali kwa mzozo uliotishia kuitumbukiza nchi hiyo katika vita vya wenyewe kwa wenyewe. Viongozi waliojitangazia wenyewe madaraka katika miji ya Slayvynsk na Donyestsk wanajiandaa kutoa taarifa kwa waandishi wa habari baada ya Putin kusema kura za maoni zinatakiwa zifutwe kuruhusu mazungumzo yafanyike.

Rais wa Uswisi, Didier Burkhalter akiwa na rais Vladimir Putin mjini Moscow
Picha: Reuters

Katika hatua ya kushangaza, rais Putin pia aliunga mkono kufanyika uchaguzi wa urais Mei 25 nchini Ukraine, jambo ambalo siku mbili kabla utawala wa Kremlin ulikuwa umelipinga kwa nguvu ukiutaja uchaguzi huo kuwa upuuzi. Mapendekezo ya Putin yametoa ishara ya kwanza ya matumaini katika kipindi cha wiki kadhaa kwamba kitisho cha kutokea vita yumkini kikaepukwa, lakini yameibua hisia mbalimbali kutoka kwa wakosoaji wa mataifa ya magharibi.

Waziri mkuu wa Ukraine, Arseniy Yatsenyuk, amemkosoa Putin kwa kuropokwa kuhusu kura za maoni za kudai uhuru, ambazo amesema kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo hazikuwa halali tangu mwanzo. Msemaji wa rais Putin ameutaka utawala wa Ukraine mjini Kiev usitishe harakati ya kijeshi dhidi ya waasi wanaoidhibiti miji kadhaa mashariki mwa Ukraine. Hata hivyo katibu wa baraza la kitaifa la usalama na ulinzi la Ukraine, Andriy Parubiy, amewaambia waandishi wa habari leo kwamba harakati hizo zitaendelea licha ya uamuzi wa kiongozi yeyote au makundi ya kigaidi katika eneo la Donetsk.

Mwandishi: Josephat Charo/AFPE/APE

Mhariri: Yusuf Saumu