Ujerumani yakamilisha kampeni kwenda Urusi kwa mafanikio
9 Oktoba 2017Ujerumani imefanikiwa kukata tikiti yake kwenda katika fainali za kombe la dunia nchini Urusi mwakani, kwa kuweka rekodi ya kufunga mabao 43 katika kipindi cha michezo ya kifuzu na kuweza kutetea ubingwa wake ilioupata nchini Brazil mwaka 2014. Ujerumani imekamilisha kampeni yake ya kufuzu kucheza katika fainali za mwakani kwa ushindi wa mabao 5-1 jana Jumapili dhidi ya Azerbaijan , lakini kocha Joachim Loew anatarajia changamoto kubwa mno katika fainali hizo.
"ni makosa kuchukulia kampeni hii ya kufuzu kucheza katika fainali kuwa kama kipimo cha ubora wa timu. Bila shaka kilikuwa kizuri , ilikuwa ni mafanikio ya wazi," Loew alisema kwa kuvunja rekodi ya Uhispania ya kufuzu kucheza katika fainali zilizofanyika nchini Afrika kusini mwaka 2010 kwa tifauti ya magoli. Lakini aliongeza kwamba "Ngazi nyingine inatusubiri katika kombe la dunia.
"Hii ndio sababu tunahitaji kutuliza boli chini, bado kuna mengi ya kufanya. Nataka kufanikisha kitu fulani kwa maana sana katika muda wa miezi michache ijayo. Itakuwa vigumu kuwa bingwa wa dunia mara mbili mfululizo , Loew alisema katika mkutano na waandishi habari.
Kwa upande mwingine mshambuliaji wa Bayern Munich Robert Lewandowski aliifungia timu yake mabao ambayo ni rekodi katika michezo ya kufuzu kucheza katika fainali za kombe la dunia wakati Poland ikiishinda Montenegro kwa mabao 4-2 na kufikia fainali hizo nchini Urusi mwakani. Lewandowski alifunga mabao 16 katika kampeni ya Poland kuelekea Urusi mwakani. Poland imefanikiwa kufunga safari kwenda katika fainali ya kombe la dunia kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2006.
England haina nafasi
England imekata tikiti yake katika fainali za kombe la dunia , lakini nafasi yake kuweza kuonesha ubavu wake nchini Urusi ni ndogo kutokana na historia yake ya hivi karibuni. Kikosi cha kocha Gareth Southgate kilikamilisha kampeni yake ya mafanikio katika kundi F kwa ushindi wa bao 1-0 nchini Lithuania jana Jumapili, na kurefusha rekodi yake ya kutofungwa katika michezo hiyo kufikia michezo 39.
Southgate hata hivyo atakuwa na matumaini madogo kutokana na kampeni hiyo , wakati England mara kadhaa imefanikiwa kufuzu katika michuano ya kufuzu , na kisha kulazimika kutolewa katika fainali katika wakati ambapo timu hiyo inamatumaini makubwa ya kusonga mbele katika fainali za kombe la dunia.
Katika historia ya miaka 51 tangu pale Uingereza iliposhinda kwa mara ya kwanza kombe la dunia katika ardhi yake, hadhi ya timu hiyo ya taifa imechafuliwa kwa kiasi kikubwa ambapo mashabiki waligeuka na kuipa mgongo wakati ilipofanikiwa kukata tikiti yake dhidi ya Slovenia siku ya Alhamis.
Wakati uwanja wa Wembley ukiwa umejaa nusu , England ilishuhudia mashabiki wakiwa hawana hamu tena kutokana na mchezo uliopooza na usio na mbinu na msisimko na kurusha mfano wa ndege ya karatasi uwanjani na kushangiria watu waliovamia uwanja.
Wachezaji nyota
Makocha wa zamani wa England waliweza kutumia kikosi chenye nyota wengi kuliko kikosi cha sasa cha Southgate , lakini kuwaita kikosini wachezaji wa nyumbani hakuna uhakika wa mafanikio. katika enzi za Sven Goran Eriksson , wachezaji kama Steven Gerrard , Frank Lampard, John Terry, Paul Scholes, David beckham na wayne Rooney walikuwa wote miongoni mwa wachezaji bora kabisa kwa vilabu vyao, wakiwa wamepata mataji pamoja na mafanikio katika Champions League.
Southgate ana kikosi ambacho hakina majina makubwa sana na uzoefu mkubwa , na hata nyota wake wakubwa Harry Kane na Dele Ali bado hawajapata tuzo kubwa katika vilabu vyao na Marcus Rashford ndio kwanza anaanza kuonesha uwezo wake.
Michezo ya kufuzu kucheza katika fainali za mwakani za kombe la dunia inaendelea tena leo ambapo Moldavia itakwaana na Austria , Wales ina miadi na Ireland, Albania itawakaribisha Wataliani mjini mwao na Ukraine itaoneshana kazi na Croatia.
Uhispania inakwaana na Israel huku mzozo wa kujitenga kwa jimbo la Catalonia ukiendelea. Hali ya hatari hata hivyo inaikabili Uholanzi. Kikosi hicho cha Wadachi kinakabiliana na Sweden kesho ambapo timu hizo zinatengana kwa pointi tatu.
Sweden ina pointi 19 , wakati Wadachi Uholanzi ina pointi 16 , na tofauti kubwa pia ya magoli. Uholanzi inahitaji kushinda mchezo huo na kupata zaidi ya mabao 7 kitu ambacho ni kigumu. Kocha wa Sweden Janne Andersson amesema.
"Ni mchezo maalum sana, na tunahisi kwamba Wadachi watacheza mchezo wa kushambulia mno, lakini tumekwisha cheza michezo kama hiyo hapo nyuma dhidi ya timu kama hizo, na Sweden itapanga mchezo wake kama inavyofikiria kwamba ni sahihi kwa hali hiyo."
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre / ape / afpe / dpa
Mhariri: Iddi Ssessanga