1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yajinowa kwa michuano ya soka bingwa wa Ulaya.

Mohamed Dahman30 Mei 2008

Nahodha wa timu ya taifa ya Ujerumani Michael Ballack ataka kikosi cha kwanza cha timu yake kupambana na Serbia katika mpambano wa kujiandaa na michuano ya soka kuwania bingwa wa Ulaya.

https://p.dw.com/p/E9H4
Michael Ballack nahodha wa timu ya taifa ya Ujerumani akizungumza na kocha wake Joachim Loew wakati wa mazoezi ya timu hiyo hivi karibuni nchini Ujerumani.Picha: AP

Nahodha wa timu ya soka ya taifa ya Ujerumani Michael Ballack amemtaka kocha Joachim Loew kuchezesha kikosi kamili dhidi ya Serbia katika mechi ya mwisho ya kujinowa kwa michuano ya mabingwa wa soka barani Ulaya inayoanza tarehe 7 Juni na kumalizika tarehe 29 Juni.

Timu ya taifa ya Ujerumani imekua ikijinowa kwa michuano hiyo inayoandaliwa kwa pamoja na Austria na Uswisi ambayo ni mikubwa kabisa na yenye msisimko wa aina yake ukiachilia ile ya kombe la soka la Dunia.

Michael Ballack ambaye pia ni mchezaji wa kiungo wa timu ya Chelsea ya Uingereza amesema mechi hiyo ya kirafiki ya kimataifa itakayochezwa leo hii dhidi ya timu ya Serbia huko Gelsenkirschen nchini Ujerumani inapaswa kucheza timu ambayo yumkini ndio itakayocheza mwezi ujao katika michuano ya mabingwa wa Ulaya badala ya kuendelea kufanya majaribio zaidi.

Amesema atafurahi na ni muhimu kwamba mechi ya mwisho kabla ya michuano ya mabingwa wa Ulaya itumike kuchezesha timu hiyo.

Kwa mujibu wa nahodha huyo wa timu ya taifa mechi za majaribio pia ni zile ambapo kikosi cha kwanza cha wachezaji 11 hujimwaga uwanjani.

Kocha wa timu ya taifa ya Ujerumani Joachim Loew amedokeza wiki hii baada ya kutangaza kikosi chake cha wachezaji 23 kwamba timu atakayoichezesha leo hii dhidi ya Serbia sio lazima iwe timu itakayopambana na Poland hapo Juni 8 huko Klagenfurt nchini Austria katika mechi ya kwanza ya Ujerumani ya michuano ya mabingwa wa Ulaya.

Kwa mara ya kwanza tokea Ujerumani ianze kuweka kambi yake ya mazoezi huko Majorca hapo tarehe 19 mwezi wa Mei Loew hapo Alhamisi tayari alikuwa na kikosi chake kamili.

Marcell Jansen ambaye alikuwa na matatizo ya misuli na mchezaji mwenzake wa timu ya Bayern Bastian Schweinsteiger ambaye aliteguka kiwiko chake cha mguu katika mechi ya Jumanne waliotoka sare ya mabao 2-2 na Belarus wote wawili wamekamilisha mazoezi.

Ballack ameonyesha kujiamini kabla ya kuanza kwa michuano hiyo ya bingwa wa Ulaya nchini Austria na Uswisi .

Ballack amesema Ujerumani ina nafasi nyengine kubwa ya kihistoria na bila ya shaka ni wazi kwamba litakuwa jambo la kufurahisha ikiwa watarudi tena walikotoka na kuweza kulinyakua taji hilo.

Nahodha huyo wa timu ya taifa ya Ujerumani mwenye umri wa miaka 31 anajiamini kwamba timu yake inaweza kuingia kwenye hatua za mtowano za michuano hiyo ya mabingwa wa soka Ulaya kwa mwaka huu wa 2008 na haitotolewa katika hatua za mwanzo kama ilivyokuwa katika michuano ya mwaka 2000 na 2004.

Amesema matarajio safari ni makubwa zaidi kuliko ilivyokuwa katika miaka ya hivi karibuni.

Mchezaji huyo anasema wanachukuwa changamoto ya kuwa miongoni mwa timu zinazowekewa matumani makubwa na kutokana na kushika nafasi ya tatu katika michuano ya Soka Kombe la Dunia mwaka 2006 haoni sababu kwa nini wasijiamini kwamba wataingia fainali.

Ujerumani itakuwa inatazamia kuboresha mchezo wake leo hii dhidi ya Serbia kuliko mechi yake iliotoka sare ya mabao 2- 2 na Belarus hapo Jumanne wakati wachezaji walipokiri kwamba walikuwa wamechoka baada ya mazoezi magumu.

Ballack amesema wachezaji inabidi wajitahidi zaidi na kodokeza kwamba timu yake itapendelea kucheza mchezo wa kujihami zaidi.

Amesema katika mchezo wake na Serbia kila kitu kitakuwa ni katika kujihami na katika mchezo na Poland hakutakuwa tena na visingizio kwamba kila mchezaji anatakiwa awe imara kabisa.

Lakini licha ya wito wa Ballack kumtaka kocha wake Loew kuchaguwa kikosi kizuri kuna masuala kwa kocha huyo juu ya uwezo wa kushambulia wa timu yake.

Mshambuliaji wa timu ya Stuttgart Mario Gomez hakuweza kushiriki mazoezi kikamilifu kwa siku 10 zilizopita wakati mshambuliaji wa Schalke Kevin Kuranyi hakuonyesha machachari ya kutosha kwenye mazoezi kuweza kuteuliwa katika kikosi cha kwanza.

Lukas Podolski mchezaji wa akiba katika timu ya Bayern Munich takriban msimu mzima,alicheza katika mechi dhidi ya Belarus na anaonyesha kuchangamka katika mazoezi jambo lililomfanya kuwa mshirika wa kawaida wa Miroslav Klose kabla na wakati wa michuano ya soka Kombe la Dunia mwaka 2006 ambapo alichaguliwa kuwa mchezaji bora mwenye umri mdogo.

Katika michuano hiyo ya ubingwa wa Ulaya Ujerumani imepangwa kwenye kundi B ambalo pia linajumuisha timu za Poland, Croatia na wenyeji wenza Austria.