Ujerumani yaifungisha virago Argentina
4 Julai 2010Ujerumani ilirudia historia, kwa kuwashinda Argentina katika robo fainali ya Kombe la Dunia kwa mara ya pili mfulilizo. Mabao manne ya Ujerumani yalitosha kumpokonya Maradona uwezekano wa kuwa mtu wa tatu katika historia kushinda taji la kombe la dunia kama mchezaji na kocha.
Thomas Mueller alifungua awamu ya mabao ya Ujerumani na baadae Miroslav Klose akafunga mabao mawili katika kipindi cha pili.
Klose sasa amefunga mabao 14 katika Kombe la Dunia. Ikiwa atafunga bao lingine moja basi atafikia rekodi ya mabao 15 iliyowekwa na Ronaldo wa Brazil.
Na katika mechi nyingine iliyochezwa hiyo jana, David Villa ndie aliyeiokoa Spain katika robo fainali ya pili, dhidi ya Paraguay.
Bao la Villa katika dakika ya 83 liliikatia Spain tiketi ya nusu fainali ya dimba la kombe la dunia kwa mara ya kwanza kabisa. Timu zote mbili zilipata mikwaju ya penalti lakini hazikuweza kufunga. Mechi ya Spain na Ujerumani itakuwa marudiano ya fainali ya Kombe la Mabingwa wa Ulaya- Spain ndio ilifanikiwa kuondoka na ushindi.
Mwandishi: Munira Muhammad/APE