Ujerumani yaibomoa Brazil na kuingia fainali!
9 Julai 2014Hicho ndicho kilikuwa kichapo kikubwa zaidi katika historia yao ya miaka 100 ya soka. Huku mchezaji wao nyota Neymar akikosekana kwa sababu ya jeraha, kila mmoja nchini Brazil alifahamu kuwa ungekuwa mtihani mkubwa kwao dhidi ya Ujerumani. Hakuna aliyetarajia matokeo ya jana. Bila shaka pengo la Thiago Silva pia lilikuwa kubwa mno na waliotwikwa mzigo wa kuliziba yaani Dante na David Luiz, walizidiwa maarifa.
Miaka 64 baada ya Brazil kutumbukia katika maombolezi ya kitaifa kufuatia kichapo walichopata katika fainali ya mwaka wa 1950, wenyeji walibomolewa katika kichapo ambacho kinaweza kuwapa msongo wa akili kuliko hata kile cha “Maracanazo”.
Nahodha wa Brazil David Luiz, huku akitiririkwa na machozi, maramoja aliomba radhi kwa taifa baada ya kipigo hicho. Kocha wake Luiz Felipe Scolari aliyeonekana kupatwa na mshangao mkubwa, aliyaunga mkono matamshi hayo akiwataka wananchi wawasamehe kutokana na makosa waliyofanya. Rais Dilma Roussef pia alituma ujumbe wa kuituliza mioyo ya mashabiki.
Thomas Müller ambaye alifunga goli lake la tano katika dimba hili, alisema hawakuamini matokeo hayo ya kushangaza. Tikiti ya Ujerumani kuelekea mjini Rio ilipatikana baada y akipindi cha kwanza cha maangamizi ambacho walifunga magoli manne katika dakika sita.
Müller alifungua ukurasa wa mabao katika dakika ya 11 kutokana na mkwaju wa kona. Miroslav Klose kisha akatia kimyani la pili katika dakika ya 23 – ambalo lilikuwa lake la 16 na kumfanya kuwa mfungaji wa magoli mengi katika historia ya Kombe la Dunia.
Kisha milango ya magoli ikafunguka. Toni Kroos alifunga mara mbili katika dakika ya 24 na 26 ili kufanya mambo kuwa 4-0 na kisha Sami Khedira akabusu wavu na kufikisha 5-0 katika dakika ya 29.
Huku wakiwa wamekufa na kuzikwa katika kipindi cha nusu saa, umati katika uwanja wa Mineirao ulibaki kimya kama maji mtungini. Mashabiki wengi walibubujikwa machozi huku wakijaribu kung'amua kilichokuwa kikitendeka uwanjani. Baada ya goli la tano, hata kabla ya kukamilika kipindi cha kwanza, mamia ya watu waliacha viti vyao na kuondoka.
Katika kipindi cha pili, Brazil ilianza kwa kishindi lakini mateso yaliendeela katika dakika ya 69 wakati Andre Schuerrle alipopachika wavuni goli. Schuerrle kisha akafunga lake la pili katika dakiak ya 79 na kufanya mambo kuwa 7-0. Goli hilo liliwafurahisha mashabiki na hata Wabrazil waliinuka na kumpongeza Schuerrle kutokana na maarifa na ujuzi aliotumia. Mara ya mwisho kupata kichapo cha aina hiyo ilikuwa mwaka wa 1920 walipozabwa magoli 6-0 na Uruguay.
Goli la dakika ya mwisho lake Oscar la kufutia machozi hata halikuwatikisa mashabiki wa Brazil ndani ya uwanja. Kocha wa Ujerumani Joachim Löw amesema Brazil walishtuka baada ya kufunwga magoli ya mapema, kwa sababu hawakutarajia hilo. Hawakujua wafanye nini. Safu yao ya ulinzi haikuwa imejipanga. Ujerumani sasa wanajiandaa kwa fainali itakayochezwa katika uwanja wa Maracana Jumapili tarehe 13. Na mpinzani wao atajulikana leo, kati ya Argentina na Uholanzi ambao wanakutana katika nusu fainali ya pili.
Mwandishi: Bruce Amani/AFP