1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yahitaji tu sare dhidi ya Denmark

16 Juni 2012

Mabingwa mara tatu Ujerumani wanaingia katika mechi ya mwisho ya kundi B Jumapili (17.06.2012) dhidi ya Denmark wakifahamu fika kuwa sare itatosha kuwapa tiketi ya kufuzu katika robo fainali

https://p.dw.com/p/15GWQ
GDANSK, POLAND - JUNE 14: Player exercise during a Germany training session at their UEFA EURO 2012 training ground ahead of their UEFA EURO 2012 Group B match against Poland, at the Germany press centre on June 14, 2012 in Gdansk, Poland. (Photo by Joern Pollex/Getty Images)
Fußball UEFA EURO 2012 Training Deutsche NationalmannschaftPicha: Getty Images

Nayo Uholanzi wakiwa ukingoni na hofu ya kuondolewa katika awamu ya makundi kwa mara ya kwanza katika miaka 32. Ujerumani inaongoza kundi hilo na pointi sita, na itapambana na Denmark iliyo na pointi tatu huku Uholanzi ambayo haina pointi yoyote ikipambana na Ureno iliyo na pointi tatu.

Beki wa Ujerumani Mats Hummels anasema inafariji sana kwamba wanahitaji tu pointi moja…Ujerumani hata hivyo haifai kukubali kushindwa goli moja kwa sifuri au magoli mawili kwa moja kwa sababu wataondolewa ikiwa Ureno itawashinda Waholanzi. Suali kubwa pekee kwa Wajerumani ni kuwa nani atakayevaa viatu vya Jerome Boateng anayetumikia adhabu ya kadi za njano. Mmoja kati ya Benedikt Hoewedes na Lars Bender atatwikwa jukumu hilo..

Beki wa Ujerumani Mats Hummels ameidhibiti vilivyo safu ya ulinzi ya timu ya Ujerumani
Beki wa Ujerumani Mats Hummels ameidhibiti vilivyo safu ya ulinzi ya timu ya UjerumaniPicha: Reuters

Denmark wanaweza kufuzu kwa awamu ya mtowano ikiwa watashinda au Uholanzi ishinde. Kwa Wadenmark, hatma yao iko mikononi mwao.

Ukraine mlima mkubwa
Ukraine wana mlima wa kupanda ili kuwashinda Uingereza na kufuzu katika robo fainali baada ya kichapo chao cha magoli mawili kwa sifuri na Ufaransa kufichua udhaifu wao katika safu ya ulinzi..

Mshambuliaji wa Ukraine Andriy Shevchenko anasema ili kuwashidna Uingereza, wanahitaji kuimarika. Shevchenko alifunga magoli mawili dhidi ya Sweden. Ukraine ambao wako nyuma ya Uingereza na alama moja, wanajua ni lazima washinde au watolewe nje ya dimba hilo.

Kurejea kwa Wayne Rooney kuna maana kuwa Roy Hodgson atachagua kikosi cha ushindi lakini hiyo itabidi amwondoe mmoja wa washambuliaji wake ambao amewasifu kwa mchezo wao.

Nahodha Andriy Shevchenko ni tegemeo la mashambulizi y Ukraine
Nahodha Andriy Shevchenko ni tegemeo la mashambulizi ya UkrainePicha: Reuters

Andy Caroll mwenye umri wa miaka 23 na Danny Welbeck mwenye miaka 21 walifunga mabao maridadi kabisa kwa njia ya kichwa na kisigino safi katika mechi ya jana dhidi ya Sweden.

Croatia yachunguzwa na UEFA
Shirikisho la soka barani Ulaya UEFA limelishitaki shirikisho la soka la Croatia kwa madai ya kibaguzi baada ya kupokea ripoti kuwa mashabiki walimkejeli mshambuliaji wa Italia Mario Balotelli kwa kuigiza milio ya tumbili.

UEFA ilipokea ripoti hizo kutoka kwa waangalizi wa kupambana na ubaguzi wa rangi walioripoti mashabiki wa Croatia wakitoa sauti za kumwiga nyani na kupeperusha bendera zenye ujumbe wa siasa kali za za mrengo wa kulia.Mashtaka hayo pia yanahusisha fataki zilizofanya mchuano kucheleweshwa.

Suala la ubaguzi lilikuwa chanzo cha hofu nchini Poland na Ukraine kabla ya dimba hilo kuanza na Balotelli alisema atamuuwa mtu atakayemrushia ndizi barabarani, au atajitoa uwanjani ikiwa atasikia kelele za kumwiga nyani wakati wa mchuano.

Mwandishi: Bruce Amani/Reuters
Mhariri: Mohamed Dahman