Ujerumani yahimili wimbi la wakimbizi
10 Septemba 2015Kwa mujibu wa Naibu Kansela wa Ujerumani Sigmar Gabriel ambaye pia ni waziri wa uchumi takriban wakimbizi 450,000 wamewasili Ujerumani hadi sasa mwaka huu wakiwemo 17,000 waliowasili katika siku nane za kwanza za mwezi wa Septemba.
Gabriel ameliambia bunge Alhamisi (10.09.2015) kwamba kufikia juzi Ujerumani imewasajili wakimbizi 450,000 wakiwemo 105,000 waliowasili mwezi wa Augusti na 37,000 waliowasili siku nane za kwanza za mwezi huu wa Septemba na kwamba yumkini mwezi huu wa Septemba idadi hiyo ya wakimbizi wanowasili nchini ikapindukia 100,000.
Serikali ya Ujerumani mapema wiki hii iliidhinisha euro bilioni 6 kugharimia wimbi la wakimbizi linalowasili nchini.Fedha hizo ni pamoja na euro bilioni 3 kwa bajeti ya mwaka 2016 na pia kusaidia kadri inavyowezekana serikali za majimbo ambazo rasilmali zao zinakabiliwa na hali ngumu kutokana na kubidi kuwahudumia wakimbizi hao.
Naibu huyo kansela amesema Ujerumani itaweza kugharamia kuwahudumia wakimbizi hao kutokana na msimao wake wa kifedha kuwa madhubuti kwa sababu ya uchumi wake kuwa na nguvu ambapo serikali inategemea utakuwa kwa asilimia 1.8 mwaka huu na mwaka ujao.
Kujumuishwa katika jamii
Gabriel amekaririwa akisema "Ni changamoto kwa Ujerumani lakini Ujeumani pia ni madhubuti.Na bila ya nchi yetu kuwa na uchumi wenye nguvu,bila ya kukuwa kwa uchumi na bila ya ajira za uhakika tusingeliweza kukabiliana na tatizo hili."
Gabriel amezisihi kampuni na wanasiasa nchini Ujerumani kuharakisha hatua za kuwajumuisha wahamiaji katika jamii kwa kuwapatia mafunzo ya kazi.Amesema wahamiaji watakuwa na manufaa kwa uchumi ambao nguvu kazi yake inategemewa kupunguwa kwa watu milioni sita ifikapo mwaka 2030.
Waziri wa Fedha wa Ujerumani Wolfgang Schauble amesema wiki hii kwamba Ujerumani inataka kuugharamia mzozo huo wa wakimbizi bila ya kuingia kwenye madeni mapya.Rasimu ya bajeti ya awali ya serikali ilikuwa euro bilioni 312 bila ya euro bilioni 6 zilizotengwa kwa wakimbizi.
Sheria kuhusu wahamiaji
Ujerumani inatarajiwa kupokea wahamiaji 800,000 mwaka huu mara nne zaidi kuliko idadi ya mwaka jana na ni kubwa zaidi kuliko idadi nyengine yoyote ile katika nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya.
Wakati huo huo polisi ya Denmark imesema haitawazuwiya tena wahamiaji na wakimbizi wanaopitia nchini humo kwenda Seweden na nchi nyengine za Scandinavia.
Hatua hiyo inaonyesha jinsi ilivyo vigumu kwa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya kuzingatia sheria ambapo kwayo watu wanaokimbia vita na ukandamizaji wanatakiwa waombe hifadhi katika nchi wanayowasili kwanza ya Umoja wa Ulaya na wasisafiri kutoka nchi moja kwenda nyengine.
Mwandishi: Mohamed Dahman/ dpa/AP/AFP
Mhariri:Yusuf Saumu