1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yaduwazwa na Poland

14 Oktoba 2014

Kocha wa Ujerumani Joachim Loew anatakiwa kuchukua hatua za haraka kubadilisha mwelekeo wa majaaliwa ya kikosi chake katika michezo ya kufuzu katika dimba la Euro 2016 nchini Ufaransa.

https://p.dw.com/p/1DVHc
EM-Qualifikation Polen - Deutschland 11.10.2014
Picha: picture-alliance/dpa/Thomas Eisenhuth

Kuteleza tena kunaweza kukiweka kikosi hicho cha Joachim Loew katika hatari kubwa kesho Jumanne dhidi ya timu kutoka Ireland ambayo ina utamaduni wa kuipa shida Ujerumani uwanjani.

Loew amesema kuwa tunapaswa kuzungumzia , vipi tunaweza kufunga mabao, kutokana na kupoteza nafasi kadhaa za kufunga mabao kama ilivyotokea katika mchezo na Poland siku ya Jumamosi , ambapo Ujerumani ilipata kipigo cha kwanza dhidi ya Poland cha mabao 2-0.

Ni kipigo cha kwanza katika michezo 33 ya kufuzu kucheza katika fainali - wakati kikosi cha kocha Loew hakikutumia fursa ilizopata. Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Ujerumani Thomas Müller anaelezea hali ya mchezo ulivyokuwa, kwa kusema."Kimchezo nadhani hali ilikuwa nzuri tu. Hususan mwishoni mwa kipindi cha kwanza hatukupata idadi kubwa ya nafasi za kupata mabao na zile chache tulizozipata hatukuzitumia. Hapa ni lazima tujilaumu wenyewe" Dakika sita baada ya kuanza kipindi cha pili , mabingwa hao wa dunia waliinamisha vichwa. Milik wa Poland alipata bao alilolifunga kwa kichwa. Mlinda mlango Manuel Neuer hakuonekana katika hali nzuri. Hii ni siku ambayo Wajerumani watapenda kuisahau haraka , lakini kwa Poland ni historia. Mchezaji wa ulinzi wa Ujerumani Mats Hummels anasema.

Joachim Löw
Kocha wa Ujerumano Joachim Löw hakuamini macho yake wakati mabingwa wa Dunia wakiadhibiwa uwanjaniPicha: picture-alliance/dpa/T. Eisenhuth

Nafikiri , tulikuwa tumeudhibiti mchezo, lakini magoli hayakupatikana kwa upande wetu. Wapinzani waliweza kufanya vizuri na hatimaye walipata ushindi wa mabao 2-0, bila shaka yoyote. Lakini hilo hutokea katika soka.

meneja wa timu ya taifa ya Ujerumani Oliver Bierhoff hata hivyo , ameonya kwamba timu yake inapaswa kuonesha nini inachoweza kufanya haraka iwezekanavyo.

EM-Qualifikation Polen - Deutschland 11.10.2014
Poland ilipata ushindi wa kihistoria dhidi ya majirani zake Ujerumani mjini WarsawPicha: Reuters/Kacper Pempel

Tunakosa hivi sasa kuchukua hatua ya mwisho. Tumegharamika , lakini sitapenda kujiweka katika mtafaruku, amesema Bierhoff jioni ya jana mjini Gelsenkirchen, ambako utafanyika mchezo kati ya Ujerumani na Ireland hapo kesho.

Kikosi cha kocha Joachim Loew kinatambua kuwa kesho dhidi ya Ireland kinapaswa kucheza kwa kiwango cha juu na tunatarajia kupata jibu sahihi. "Mafanikio katika kupata magoli, hayana mahusiano na mbinyo uliopo. Hatuhitaji pia kufanya maajabu wakati wa matayarisho katika chumba cha kuvalia. Hii ni kitu ambacho kinaambatana na jinsi tunavyofikiri, ambapo nina maana kwamba kuna kitu kinakosekana katika umaliziaji".

Ujerumani inakumbana na Ireland leo Jumanne mjini Gelsenkirschen , wakati kikosi cha Martin O'Neill kikitafuta kwa mara ya kwanza kupata ushindi dhidi ya mabingwa hao wa dunia katika muda wa miaka 20.

Ireland ilipata ushindi dhidi ya Ujerumani wa mabao 2-0 Mei mwaka 1994 wakati Tony Cascarino na Rary Kelly walipoipatia Ireland mabao mjini Hannover katika mchezo wa kirafiki na kikosi hicho kinamatumaini ya kuwafumania wenyeji wao wakiwa bado hawajaamka baada ya kipigo dhidi ya Poland. Kwa kulinganisha Ireland inajiamini baada ya kuirarua Gilbralter kwa mabao 7-0 mjini Dublin na kuchupa hadi nafasi ya pili katika kundi D nyuma ya viongozi wa kundi hilo Poland.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / rtre / dpa
Mhariri: Yusuf Saumu