Ujerumani yachukua urais wa baraza la Umoja wa Ulaya
1 Julai 2020Ujerumani Jumatano inachukua urais wa kupokezana wa baraza la Umoja wa Ulaya kwa muda wa miezi sita, ikilenga kukabiliana na janga la virusi vya corona na kuokoa uchumi.
Ikipokea kijiti hicho kutoka Croatia, Ujerumani itaandaa na kuongoza mikutano baina ya wakuu wa serikali wa Umoja wa Ulaya na mawaziri, chini ya kauli mbiu pamoja kwa mustakabli wa Ulaya.
Awali Ujerumani ilikuwa imepanga kujikita katika ulinzi wa mipaka wa Umoja wa Ulaya, mahusiano yake na China na suala la mabadiliko ya tabia nchi, lakini janga la mripuko wa virusi vya korona, umelilazimu taifa hilo lenye nguvu kiuchumi, kujielekeza katika kushughulikia mgogoro wa COVID-19.
Changamoto ya kwanza ya Ujerumani itakuwa ni kusimamia upitishwaji wa mfumo wa kifedha wa miaka saba wa Umoja wa Ulaya, na jukumu la maamuzi kwenye majadiliano ya uhusiano mpya wa kibiashara na Uingereza.
Chanzo: dpae