Ujerumani yachukua hatua kali kupambana na COVID-19
27 Agosti 2020Hayo yote yanafanyika katika hatua za kukabiliana na ongezeko la maambukizi ya virusi vya corona. Viongozi hao wa Ujerumani wametangaza kuongeza marufuku ya matukio makubwa ya umma kama vile matamasha ya muziki hadi mwishoni mwa mwaka, kama sehemu ya hatua inayolenga kupunguza maambukizi ya virusi vya corona nchini Ujerumani.
Mkutano wa kwanza kufanyika tangu Juni
Hatua hiyo imefikiwa katika mkutano uliofanyika Alhamisi kwa njia ya video na kuhudhuriwa na Kansela Merkel na viongozi wa majimbo hayo, ukiwa ni wa kwanza kufanyika tangu Juni 17.
Hatua nyingine zilizochukuliwa ni kuanzishwa kwa faini ya kitaifa ya kiwango cha chini cha euro 50, kwa watu watakaokataa kufuata masharti ya kuvaa barakoa kwenye maduka na usafiri wa umma.
Hata hivyo, Waziri Mkuu wa jimbo la Saxony-Anhalt, Reiner Haselhoff ambaye jana Jumatano jimbo hilo lilirekodi visa vipya 16 vya virusi vya corona, amekataa kukubali faini ya kiwango cha chini na amesema jimbo lake halitosaini kuitekeleza sheria hiyo mpya.
Viongozi hao wameweka masharti kwenye mikusanyiko midogo, ambapo shughuli binafsi zinapaswa kuwa na watu 25, huku sherehe zitakazofanyika nje ya nyumba za kuishi zinaruhusiwa kuwa na watu 50.
Pendekezo la Spahn laungwa mkono
Merkel pia ameunga mkono pendekezo la Waziri wa Afya wa Ujerumani, Jens Spahn la kusitisha kuwapima bure virusi vya corona watu wanaorejea Ujerumani kutoka nje ya nchi. Upimaji wa bure wa virusi vya corona utamalizika Septemba 15. Hata hivyo, hii haitawahusu wale wanaorejea kutoka kwenye maeneo yenye hatari kubwa zaidi, kwani watalazimika kujiweka karantini kwa siku 14.
Spahn amesema baada ya kumalizika kwa msimu wa safari, maafisa wanatarajiwa kutekeleza masharti ya karantini kwa watu wanaoingia kutoka kwenye maeneo hatari zaidi.
''Wakati ambao idadi ya maambukizi Ujerumani ilikuwa chini, ni muhimu kuzuia virusi visisambae nchini kupitia wafasiri wanaorejea. Kwa hivyo tunalazimika kubadili mfumo wa upimaji kulingana na hali hiyo,'' alifafanua Spahn.
Waziri Mkuu wa jimbo la Bavaria, Markus Soeder ni mmoja wa walioupinga mpango huo. Amesema upimaji ulianzishwa wiki mbili tu zilizopita na sasa unaondolewa tena. Soeder amebainisha kuwa badala yake serikali kuu ya Ujerumani inapaswa kuongeza uwezo wake wa kuwapima watu virusi vya corona.
Hata hivyo, Waziri Mkuu wa jimbo la Schleswig-Holstein, Daniel Guenther ameliunga mkono pendekezo la Waziri Spahn, akisema uwezo uliopo ni mdogo, hivyo hawawezi kuwapima watu bila ubaguzi.
Siku ya Alhamisi taasisi ya kudhibiti magonjwa ya Ujerumani, Robert Koch imerekodi ongezeko la visa 1,507 vya virusi vya corona na kuifanya idadi jumla kufikia 237,936. Mwishoni mwa wiki iliyopita maambukizi yalizidi 2,000 idadi ya juu kushuhudiwa tangu mwishoni mwa mwezi Aprili.
(DPA)