1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yaapa kulipa kisasi kwa kufungwa na Uhispania katika fainali ya Ulaya mwaka 2008

7 Julai 2010

Wachezaji wa Ujerumani wawindwa na vilabu kadhaa barani Ulaya

https://p.dw.com/p/ODA2
Nahodha wa Ujerumani aliyezikosa fainali za mwaka huu nchini Afrika kuisni,Michael Ballack, kushoto,akishangilia bao wakati akiichezea Ujerumani pamoja na kiungo aliyepewa majukumu ya kuziba nafasi hiyo kwa sasa Bastian Schweinsteiger.Schweinsteiger kwa sasa anawindwa na vilabu kadhaa barani Ulaya,ikiwemo Real Madrid ya Uhispania. Kiungo huyoPicha: AP

Baada ya Uholanzi hapo jana kukata tiketi ya kuwa timu ya kwanza kutinga fainali ya kombe la dunia,ili kutimiza kiu yake ya kulitwaa kombe hilo alau mara moja,macho na masikio ya mashabiki wa soka ulimwenguni,sasa yanaukodolea mpambano baina ya Ujerumani na Uhispania,katika nusu fainali ya pili,usiku huu.

Ujerumani inayotumia mfumo wa ukabaji wa kiitali,kasi ya Kiingereza,na mchezo wa pasi za haraka haraka wa kihispania,imedhamiria mwaka huu sio tu kufika fainali,lakini pia kulipa kisasi cha kufungwa na Uhispania,katika fainali za Ulaya mwaka 2008,na kutawazwa mabingwa wa michuano hiyo.

Tayari kocha wa Uhispania,Vicente Del Bosque amekimwagia sifa kikosi cha vijana wa Ujerumani kwa kucheza soka la kisasa na lenye mfumo unaoeleweka,lakini ameweka wazi kuwa licha ya kumtegemea David Villa katika safu ya ushambuliaji,na kuwa na idadi ndogo ya mabao ya kufunga,leo lazima waing´oe Ujerumani na kutinga fainali.

Timu hizo mbili,zote zimeshaonja chungu ya kufungwa katika michuano ya mwaka huu,ambapo Ujerumani ilikubali kuchapwa bao 1-0 na Serbia,wakati Uhispania ilipoteza mchezo wa kwanza dhidi ya Uswizi katika hatua za makundi.

Hata hivyo,wachambuzi wa masuala ya kandanda wanaipa nafasi kubwa Ujerumani,kutokana na kutoa vipigo vya kufedhehesha kwa idadi ya mabao manne,kwa timu za Australia,Uingereza na Argentina,lakini inaelezwa kuwa kukosekana kwa Thomas Muller,kunaweza kupunguza kasi ya kushambulia ya timu hiyo.

Kwa upande mwingine,washambuliaji David Villa wa Uhispania,na Miroslav Klose wao leo hii,watakuwa na vita nyingine tofauti,wakati David Villa anawania kiatu cha dhahabu cha ufungaji bora,Klose yeye anawania kufuta rekodi ya magoli mengi yaliyofungwa na Ronaldo De Lima wa Brazil,na kutawazwa mwamba wa kuzifumania nyavu tangu kuanza kwa michuano ya kombe la dunia.

Ronaldo ameshafunga mabao 15 mpaka sasa,ambapo Klose anahitaji bao 1,ili kufikia rekodi hiyo.

Uhispania licha ya kuanza michuano hii kwa kusuasua,imeanza kurudia kiwango chake cha kutandaza soka la kuvutia,ikiwatumia viungo Andres Inniesta na Xavi Hernandez wa Barcelona,hali inaoelezwa kuweza kuleta ladha ya mchezo wa leo ambapo Ujerumani,imekuwa imara zaidi katika safu hiyo,inayoongozwa na Bastian Schweinsteiger na Sami Khedira.

Tayari viungo hao wawili wameshaandaliwa donge nono na Real Madrid kwa ajili ya msimu ujao,lakini Bayern Munich imeshakataa kumuuza Schweinsteiger.

Sami Khedira,aliyekuwa nahodha wa timu ya vijana ya Ujerumani iliyotwaa ubingwa wa Ulaya,pia anasakwa kwa udi na uvumba na klabu ya Chelsea ya Uingereza,kwa sasa anachezea klabu ya Stutgart ya hapa Ujerumani.

Tayari kombe hilo,limeshawekwa rehani na Italia,ambayo ilikubali kufungasha virago mapema,hivyo kwa mara nyingine,litaendelea kubakia Ulaya,kutokana na kuwa na uhakika wa kuingiza timu mbili katika fainali ya mwaka huu kutoka bara la Ulaya,kabla ya kwenda kulitetea kombe hilo huko Brazil,katika fainali zijazo za kombe la dunia mwaka 2014.

Wakati huo huo,kambi ya timu ya Ujerumani nusura iingie dosari baada ya kuzuka kwa tafrani,baina ya nahodha wa zamani,Michael Ballack na wa sasa Philip Lahm,aliyeeleza wazi kuwa hatokuwa radhi kumpa nafasi hiyo Ballack,baada ya kupona majeraha.

Hata hivyo,mzozo huo kwa sasa umemalizwa,na kambi ya timu hiyo imethibitisha kwamba mkakati wao ni kuifunga Uhispania,na kuingia fainali.

Mwandishi; Ramadhan Tuwa/ AFP/DPA

Mhariri;Abdul-Rahman