1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yaanza vizuri michuano ya Euro 2016

8 Septemba 2014

Mabingwa wa dunia Ujerumani yapata ushindi wa taabu dhidi ya Scotland katika michuano ya kuwania tikiti ya kucheza katika fainali za kombe la mataifa ya Ulaya , Euro 2016 nchini Ufaransa.

https://p.dw.com/p/1D8vl
EURO 2016 Qualifikation Deutschland vs Schottland
Die Manschaft , timu ya UjerumaniPicha: picture-alliance/dpa

Uingereza inaanza kampeni yake leo(08.09.2014) dhidi ya Uswisi, na Uhispania ina miadi na Macedonia jioni ya leo.

Mchezaji wa kati wa timu ya taifa ya Ujerumani Die Manschaft , Thomas Mueller alipachika mabao mawili muhimu jana na kuzindua kwa mafanikio kampeni ya mabingwa hao wa dunia ya kuwania kukata tikiti ya kucheza katika fainali za kombe la mataifa ya Ulaya , Euro 2016 nchini Ufaransa kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Scotland jana Jumapili katika kundi D.

EURO 2016 Qualifikation Deutschland vs Schottland
Ikechi Anya wa Scotland akishangiria bao la kusawazisha dhidi ya UjerumaniPicha: Simon Hofmann/Bongarts/Getty Images

Mueller alifungua ukurasa wa mabao katika dakika ya 18 kwa kichwa, lakini Ikechi Anya wa Scotland alirejesha bao hilo katika dakika ya 66 ya mchezo huo.

Matarajio ya Scotland ya angalau kupata point moja yalifutika wakati Mueller alipoweka wavuni bao ambalo lilionekana kuwa ndio la ushindi dakika nne tu baadaye.

Kocha wa Ujerumani amesema baada ya mchezo huo kuwa , "Nimeridhika na point tatu. Ilikuwa ni muhimu kuanza na ushindi," amesema kocha Joachim Loew, ambaye kikosi chake hakijashindwa katika michezo 33 ya mashindano ya Ulaya ama michezo ya kuwania kufuzu katika kombe la dunia. Mfungaji wa mabao hayo Thomas Mueller alisema.

"Ni dhahiri kuwa mtu hufurahi , iwapo anafunga bao. Lakini mtu hufurahi zaidi , iwapo pia bao hilo linatosha kwa ushindi. Na Namshukuru Mungu kwamba hilo limetokea na imetosha , na natambua ni muhimu namna gani point hizi tatu kwetu na kwamba sasa hakuna anayeweza kutupita."

EURO 2016 Qualifikation Deutschland vs Schottland
Thomas Mueller wa Ujerumani (kulia)Picha: picture-alliance/dpa

Mueller alipoteza nafasi mbili nzuri za kupata mabao kabla ya kutumia nafasi ya tatu kuweka bao muhimu kwa mabingwa hao wa dunia wakati Waskochi walipoibana Ujerumani katika kipindi cha pili, kama anavyothibitisha mshambuliaji wa Ujerumani Lukas Podolski.

"Ilikuwa kibarua kigumu kupata ushindi huu, points tatu tumeziweka kibindoni, na hilo ndio muhimu zaidi hatimaye. Na utaona kwamba , timu za miaka huenda kumi, ama kumi na tano iliyopita, zingeelezwa kwa ushindi huu kuwa kila kitu kimekamilika, na ziko miongoni mwa timu za juu. Na hii imetulazimu kujituma zaidi hii leo. lakini pia ni lazima kuipongeza timu ya Scotland , kwani imecheza soka safi na kupambana kiume. Lakini hatimaye tumepata point tatu na hilo ndio muhimu zaidi."

Mbali ya kuipa Scotland pongezi kwa kutoa changamoto kubwa dhidi ya mabingwa hao wa dunia ,a lakini mlinda mlango wa Ujerumani Manuel Neuer, amesema Ujerumani ilipoteza udhibiti wa mchezo huo katika kipindi cha pili.

Fußball WM 2014 Halbfinale Deutschland Brasilien Neuer
Manuel Neuer mlinda mlango wa UjerumaniPicha: Reuters

"Tulianza vizuri kwa hakika. Kipindi cha kwanza kila kitu kilikuwa mikononi mwetu. Tulicheza vizuri na katika kipindi cha kwanza kila kitu kilikwenda vizuri. Bahati mbaya katika kipindi cha pili hatukuanza vizuri sana, kama ilivyokuwa katika kipindi cha kwanza , na tunaweza kusema , kwamba tulishindwa kupata bao la pili na tukafanya makosa kadhaa katika kujenga mashambulizi yetu. Na ndio Waskochi wakaanza kucheza kwa kushambulia kwa kushitukiza, kama ilivyoonekana."

Katika wapinzani wengine wa kundi la Ujerumani la D, Poland jana iliishindia Gibraltar kwa mabao 7-0 na Ireland ikaishinda Georgia kwa mabao 2-1 pia.

Marco Reus kukaa nje ya uwanja mwezi mmoja

Wakati huo huo mchezaji wa kiungo wa Ujerumani Marco Reus , ambaye amekosa kucheza katika fainali za kombe la dunia kwa maumivu ya kifundo cha mguu , amepata maumivu tena katika sehemu hiyo hiyo jana na kocha Joachim Loew anatarajia kuwa maumivu hayo si makubwa hivyo.

Kocha wa Uingereza Roy Hodgson amesema jana kuwa angependelea mchezo wa leo wa ufunguzi wa kampeni ya timu yake katika fainali za kombe la mataifa ya Ulaya kutoka kundi E dhidi ya Uswisi ungekuwa baadaye na sio wakati huu.

Interaktiver WM-Check 2014 Trainer England Hodgson
Kocha wa Uingereza Roy HodgsonPicha: Getty Images

Uingereza inapambana na Uswisi leo(08.09.2014) katika mchezo wa kuwania kufuzu kucheza katika fainali za kombe la mataifa ya Ulaya , Euro 2016 nchini Ufaransa. Hali ya kujisikia kushindwa bado inaizunguka Uingereza baada ya kufanya vibaya katika fainali za kombe la dunia nchini Brazil mwezi Juni , wakati kikosi hicho kilipoambulia point moja tu katika michezo mitatu, na hali hiyo haikuweza kutoweka hata baada ya ushindi wa bao 1-0 katika mchezo wa kirafiki dhidi ya Norway Jumatano wiki iliyopita.

Kocha atamba

Kocha wa Uswisi Vladimir Petkovic amesema jana kuwa kikosi chake kitaingia dimbani kukabiliana na Uingereza katika hali ya usawa.

Michezo mingine ni kati ya Uhispania inayopambana na Macedonia leo , ambapo kocha wa Uhispania Vicente del Bosque amesema anaendelea kumuamini mlinda mlango Iker Casillas kwa ajili ya mchezo huo wa kwanza wa kikosi chake.

Uholanzi chini ya kocha mpya Guus Hiddink wananza kampeni yao dhidi ya jamhuri ya Czech kesho Jumanne(09.09.2014).

Uholanzi imebadilisha kocha baada ya kocha Louis van Gaal kutimkia Machester United na kumpa wadhifa huo Guus Hiddink.

Lakini enzi mpya na kocha mpya Guus Hiddink iliwatumbukia nyongo wakati walipocharazwa mabao 2-0 na Italia katika mchezo wa kirafiki mjini Bari siku ya Alhamis.

Mabingwa wa Afrika Nigeria waangukia pua

Katika bara la Afrika mabingwa watetezi wa kombe la mataifa ya Afrika Nigeria ilipoteza mchezo wake dhidi ya jamhuri ya Kongo siku ya Jumamosi mwanzoni mwa michuano ya kuwania kufuzu kucheza katika fainali za kombe la mataifa ya Afrika mwakani nchini Morocco.

Cote D'Ivoire ilikuwa nyuma kwa bao 1-0 lakini ilifanikiwa hatimaye kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Sierra Leone , na Ghana ilibidi kupambana kiime na kupata sare ya bao 1-1 nyumbani dhidi ya Uganda . Cameroon na Algeria , wawakilishi wengine wawili wa Afrika katika fainali za kombe la dunia zote zilipata ushindi.

Hali ya kusuasua imeendelea hivi karibuni kwa Nigeria , huku nchi hiyo ikikabiliwa na kitisho cha kuzuiwa kushiriki michezo ya kimataifa na shirikisho la soka duniani FIFA kwasababu ya matatizo na shirikisho la kandanda nchini humo na bado wanavutana kuhusu mkataba mpya ndani ya shirikisho hilo kuhusu mkataba wa kocha Stephen Keshi.

Sepp Blatter Sao Paulo
Rais wa FIFA Sepp BlatterPicha: NELSON ALMEIDA/AFP/Getty Images

Blatter kuwania muhula mwingine

Rais wa shirikisho la kandanda duniani FIFA Sepp Blatter amethibitisha kuwa atagombea wadhifa huo tena katika uchaguzi mwakani. Blatter mwenye umri wa miaka 78 raia wa Uswisi , ambaye alichaguliwa mara ya mwanzo mwaka 1998, amethibitisha kugombea katika taarifa iliyotolewa kwa wajumbe wa mkutano wa Soccerex Global mjini Manchester nchini Uingereza leo.

Na katika mpira ya kikapu, Uturuki imeiangusha Australia kwa vikapu 65-64 katika michuano ya kombe la dunia la mchezo huo mjini Barcelona , Uhispania.

Uturuki sasa itacheza na Lithuania kesho Jumanne baada ya Lithuania kupata ushindi wa vikapu 76-71 dhidi ya New Zealand.

Brazil ikaishinda Argentina kwa vikapu 85-65 katika pambano la mahasimu ya Amerika ya kusini. serbia inaisubiri Brazil kwa hiyo siku ya Jumatano baada ya timu hiyo kuiangusha Ugiriki kwa vikapu 90-72.

Tennis Australian Open Serena Williams
Serena Williams bingwa wa US OpenPicha: Reuters

Na hatiamaye Tennis.

Serena Williams ameingia katika vitabu vya historia ya mchezo huo duniani jana baada ya kunyakua ubingwa wake wa 18 wa Grand Slam kwa kupata ushindi wa sita wa mashindano ya tennis ya US Open jana Jumapili.

Mafanikio hayo dhidi ya Caroline Wozniacki umemfikisha bingwa huyo pamoja na mabingwa wa zamani Chris Evert na Martina Navratilova katika nafasi moja ya kunyakua mataji katika mashindano makubwa manne ya mchezo huo duniani.

Mwandishi: Sekione Kitojo / ape / dpae / afpe

Leo hii Uingereza