Ujerumani yaamua kuwapa silaha Wakurdi wa kaskazini mwa Irak
21 Agosti 2014Serikali ya Ujerumani inautayarisha mpango wa kuwapekelea silaha wa Wakurdi wa kaskazini mwa Irak wanaopambana na wapiganaji wa kundi la kigaidi la Waislamu wenye itikadi kali, IS ambao kwa sasa wanayashikilia maeneo kadhaa nchini Irak na Syria. Waziri wa mambo ya nje Frank - Walter Steinemeier amesema Ujerumani itapima kwa makini ili kubainisha ni silaha za aina gani zinazostahili kupelekwa kwa Wakurdi wa kaskazini mwa Irak.
Licha ya wanasiasa wa upinzani kuupinga uamuzi huo,Waziri Steinmeier na Waziri wa ulinzi Ursula von der Leyen wamekubaliana na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel juu ya kuwasaidia Wakurdi kwa kuwapa silaha.
Hata hivyo Waziri Steinmeier amewaambia waandishi habari mjini Berlin kuwa Ujerumani itashirikiana kwa undani na Ufaransa,Uingereza,Italia na nchi nyingine za Ulaya ambazo pia zipo tayari kuwapa silaha Wakurdi wa Irak.
Makombora ya kuteketezea virafu
Mjumbe wa kamati ya masuala ya nje ya chama cha CDU kinachoiongoza serikali ya mseto nchini Ujerumani bwana Philipp Mißfelder ameeleza kwamba alipokea maombi kutoka kwa wawakilishi wa Wakurdi ya kupatiwa haraka makombora ya kuteketezea vifaru. Amesema ni jambo la lazima kuyazingatia maombi hayo ili kuwakabili na kuwakomesha wapiganaji wa dola ya kiislamu IS. Hata hivyo Bunge la Ujerumani litapaswa lishiriki katika kutoa idhini ya kuwapatia Wakurdi wa kaskazini mwa Irak roketi hizo aina ya Milan.
Lakini kiongozi wa wabunge wa chama cha upinzani cha kijani Katrin Göring -Eckardt ameukosoa uamuzi huo. Hatahivyo amesema ridhaa ya Bunge itahitajika ili uweze kutekelezwa.
Umoja wa Mataifa pia wasaidia
Wakati huo huo Umoja wa Mataifa umeanza kuutekeleza mpango kabambe wa kupeleka misaada ya kibinadamu kwa watu nusu Milioni wa kaskazini mwa Irak. Maalfu ya watu hao wameyakimbia makaazi yao baada ya wapiganaji wa dola ya kiislamu ,IS kuziteka sehemu za kaskazini na kusini mwa Irak mnamo mwezi wa Juni. Ndege ya kwanza kutokea Jordan imetua Arbil, mji mkuu wa jimbo la Wakurdi, ikiwa na shehena ya tani 100 za misaada ya dharura.
Mwandishi habari wa Marekani achinjwa
Na habari kutoka Washington zinasema Shirika la FBI limethibitisha kwamba ukanda wa video uliotolewa na dola ya kiislamu ni wa kweli. Ukanda huo unaonyesha jinsi mwandishi habari wa Marekani James Foley anavyochinjwa.
Mwandishi:Mtullya Abdu. ZA/epd,afp,
Mhariri: Yusuf Saumu