1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yaadhimisha miaka 65 kukumbuka jaribio la kutaka kuuawa Adolf Hitler

Kabogo Grace Patricia20 Julai 2009

Katika kuadhimisha siku hii, makuruta 400 huapishwa ili kuhudumia Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani kwa uaminifu.

https://p.dw.com/p/ItMI
Kiongozi wa utawala wa kifashisti, Adolf HitlerPicha: PA/dpa


Ujerumani leo inaadhimisha miaka 65 kukumbuka jaribio la kutaka kumuua Adolf Hitler katika makao makuu ya jeshi, mwaka 1944, ambalo halikufanikiwa.

Katika jaribio hilo la mauaji la Julai 20, mwaka 1944, afisa wa juu wa jeshi, Claus von Stauffenberg, alitega bomu chini ya meza katika mkutano uliofanyika Prussia Mashariki, ambayo ni Poland ya sasa. Von Stauffenberg, baada ya hapo aliondoka katika chumba hicho cha mkutano kabla ya bomu kuripuka. Baada ya kusikia mripuko, alidhania kuwa Hitler amekufa na aliondoka kwenda Berlin, ambako yeye pamoja na kundi lake la maafisa wa ngazi ya juu wa utawala wa kijeshi walipanga kuuangusha madarakani utawala wa Hitler.

Lakini afisa mmoja aliuondoa mkoba uliokuwa na bomu hilo na Hitler alisalimika kwa kupata majeraha madogo kufuatia kuripuka kwa bomu hilo. Von Stauffenberg na wenzake waliuawa kwa kupigwa risasi, muda mfupi baadae katika eneo ambalo bado ni sehemu ya wizara ya ulinzi na sehemu ya ukumbusho ambako shughuli za kuweka mashada ya maua zimefanyika.

Baadae leo Waziri wa uchumi wa Ujerumani, Karl-Theodore zu Guttenberg, anatarajiwa kuzungumza katika maadhimisho hayo kwenye viwanja vya kumbukumbu kaskazini mwa Berlin lilipokuwa gereza la zamani, ambako kiasi cha watu 90 wanaotuhumiwa kuhusika katika jaribio hilo la mauaji, waliuliwa.

Aidha, katika kuadhimisha siku hii ya leo, makuruti wapya 400 wa kikosi cha walinzi wataapishwa rasmi uwanjani mbele ya Bunge, Reichstag, kuhudumia Shirikisho la Jamhuri ya Ujerumani kwa uaminifu na kulinda kishujaa haki na uhuru wa umma wa Ujerumani.

Mwaka jana, kwa mara ya kwanza, waziri wa ulinzi wa Ujerumani, Franz Josef Jung, aliamua kuifanya sherehe hiyo katika uwanja ulio mbele ya jengo la bunge. Hapo zamani sherehe hiyo ilifanywa mbele ya jengo la wizara ya ulinzi. Hatua ya kuhamisha sherehe hiyo karibu na bunge la Ujerumani, inasisitiza mfungamano wa karibu uliokuwepo kati ya bunge na jeshi la Ujerumani.

Mwaka huu makuruti hao wapya watahutubiwa pia na Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, mbali na ilivyo kawaida kwa waziri wa ulinzi kufanya hivyo.

Makuruti huapishwa kila Julai 20, kuwaheshimu maafisa waliojaribu kumuua Hitler bila mafanikio. Mfano wa maafisa hao unapaswa kuwa kigezo kwa wanajeshi vijana.

Mwandishi: Grace Patricia kabogo (AFPE)

Mhariri: Miraji Othman