1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani, Uholanzi, Austria, Croatia zatinga Euro 2020

17 Novemba 2019

Ujerumani, Uholanzi, Austria na Croatia zimetinga katika mashindano ya ubingwa wa Ulaya mwaka ujao jana usiku. Wajerumani watashiriki Euro 2020 kwa mara ya 13.

https://p.dw.com/p/3TAkb
Fussball UEFA EM 2020 Qualifikation l Deutschland vs Weißrussland l 3:0 Jubel Toni Kroos
Picha: Reuters/Schmuelgen

Mabingwa hao mara tatu walijikatia tiketi baada ya kuwazaba Belarus mabao manne kwa sifuri, huku Toni Kroos akifunga mawili na kuiongoza timu yake kukamata usukani wa Kundi C.

Nambari mbili Uholanzi pia ilifuzu licha ya kutoka sare tasa na Ireland Kaskazini mjini Belfast. Nahodha wa Ireland Kaskazini Steven Davis alipoteza penalti katika kipindi cha kwanza. Kwa Waholanzi, itakuwa mara yao ya kwanza kushiriki mashindano makubwa tangu Kombe la Dunia 2014. Austria waliungana na Poland ambao tayari wamefuzu katika Kundi G kwa ushindi wa 2 - 1 dhidi ya Macedonia Kaskazini. Poland ilishinda 2 - 1 katika ushindi wao wa kwanza nchini Israel tangu 1998. Croatia walifuzu kama washindi wa Kundi E kwa ushindi wa 3 -1 dhidi ya Slovakia.

Ujerumani ambayo inakumbwa na majeruhi kikosini, ilianza na safu ya ulinzi isiyo ya kawaida ambapo Matthias Ginter wa Borussia Moenchengladbach alipangwa na Robin Koch wa Freiburg. Ilikuwa mechi ya pili kwa Koch katika timu ya taifa nay a kwanza ya ushindani. Safu ya mashambulizi ya timu hiyo ya Joachim Loew ilikuwa moto wa kuotewa mbali huku Timo Werner, Serge Gnabry na Toni Kroos wakitamba.

Ujerumani ilipata bao la kwanza kupitia Ginter katika dakika ya 41, Leon Goretzka akafunga dakika nne baada ya kipindi cha pili kuanza. Kroos akatupa kambani bao la tatu baada ya kuandaliwa pasi na Ginter katika dakika ya 55. Manuel Neuer aliokoa penalty ya Belarus kabla ya Kroos kufunga kazi kwa kutikisa wavu kwa mara ya pili katika ya 83.