1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani, Uhispania, Sweden zataka kupunguzwa nyuklia

5 Julai 2021

Mawaziri wa Mambo ya Kigeni wa Ujerumani, Uhispania na Sweden wametoa wito kwa mataifa yote yenye nguvu duniani yanayomiliki silaha za nyuklia kupunguza kwa kiasi kikubwa zana zao.

https://p.dw.com/p/3w3ad
Spanien Madrid | Ministertreffen der Stockholm-Initiative fuer nukleare Abrüstung |Ann  Linde, Heiko Maa und Arancha González
Picha: Thomas Imo/photothek/imago images

Mawaziri hao Heiko Maas wa Ujerumani, Arancha Gonzalez Laya wa Uhispania na Ann Linde wa Sweden wameandika kwenye toleo la leo la gazeti la Ujerumani la Rheinische Post kuwa madola yenye nguvu yanaweza yakuchukua hatua zikiwemo kupunguza mchango wa silaha za nyuklia katika mikakati na sera, kupunguza kitisho cha migogoro na kutumiwa kwa bahati mbaya kwa silaha ya nyuklia, kupunguza zaidi hifadhi za nyuklia na kuweka misingi kwa ajili ya kizazi kipya cha makubaliano ya kudhibiti silaha.

Wamesema lazima wakomeshe kabisa majaribio ya silaha za nyuklia kwa hatimaye kuanza kuutekeleza Muafaka wa Kupiga Maerufuku Majiribio ya Nyuklia, kuanzisha upya mazungumzo ya mkataba unaopiga marufuku utengenezaji wa nyenzo za nyuklia kwa ajili ya matumizi ya kijeshi na kujenga uwezo mkubwa na wa kuaminika wa kuthibitisha hatua za kuwachana na nyuklia.

Spanien Madrid | Ministertreffen der Stockholm-Initiative fuer nukleare Abrüstung | Heiko Maas
Waziri Maas wa Ujerumani kwenye mkutano wa MadridPicha: Thomas Imo/photothek/imago images

Mkutano unafanyika leo chini ya Mpango wa Stockholm, ambao unazileta pamoja nchi 16 zinazoshinikiza kupigwa hatua katika kupunguzwa kwa zana za nyuklia duniani kote.

Mkutano wa Rais Joe Biden wa Marekani na Vladmir Putin wa Urusi katikati ya mwezi Juni ulifufua matumaini ya kupigwa hatua. Madola hayo mawili yenye nguvu duniani yenye silaha za nyuklia yalikubaliana kuhusu mazungumzo ya kuondolewa silaha za nyuklia.

Taasisi ya amani ya SIPRI yenye makao yake mjini Stockholm ilitoa ripoti katikati ya Juni iliyoonyesha kuwa kulikuwa na kiwango cha jumla cha kupungua kwa idadi ya vichwa vya nyuklia katika mwaka wa 2020, lakini Zaidi vilitumiwa na wanajeshi walioko kwenye operesheni.

Na wakati mkutano huo ukiendelea Madrid, kiwanda pekee cha umeme wa nyuklia nchini Iran kimeanza tena kufanya kazi, baada ya wiki mbili za kuwa gizani wakati kukiwa na uhaba wa umeme kote katika Jamhuri hiyo ya Kiislamu. Kufungwa kwa kiwanda hicho cha Bushehr awali kulitokana na kile kilichosemekana kuwa ni hitilafu ya kiufundi ambayo ilihitaji marekebisho kufuatia ripoti za kukanganyana kuwa ilikuwa operesheni ya kila mara ya matengenezo.

DPA