1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani, Ubelgiji, na Uswisi zatua Brazil

12 Oktoba 2013

Ujerumani, Ubelgiji na Uswisi zimejikatia tikiti za kuingia katika dimba la kombe la Dunia nchini Brazil, wakati Uhispania, England na Urusi pia zikishinda mechi zao hapo jana ili kuweka hatima zao mikononi mwao

https://p.dw.com/p/19yNy
Mesut Özil (kulia) aking'ang'ania mpira na mchezaji wa Ireland Simon Cox
Mesut Özil (kulia) aking'ang'ania mpira na mchezaji wa Ireland Simon CoxPicha: picture-alliance/dpa

Kinyang'anyiro cha mwaka ujao, pia kinaonekana kukaribiwa na Bosnia-Herzegovina, ambayo haijawahi kucheza katika Kombe la Dunia, lakini Christiano Ronaldo anaonekana kuingia katika duru ya mchujo pamoja na timu yake ya Ureno, baada ya usiku ambao picha kamili ya kufuzu katika makundi yote 9 ilijitokeza wazi.

Uholanzi ambayo tayari ilijikuwa imejikatia tikiti ya Kombe la Dunia kabla ya kuichabanga Hungary mabao manane kwa moja, ikiwa ni pamoja na mabao matatu kutoka kwa Robin van Persie ambayo yalimweka mshambuliaji huyo wa Manchester United juu ya chati ya mfungaji wa mabao mengi nchini mwake, akiwa na 41.

Ujerumani ilipata ushindi rahisi wa mabao matatu kwa sifuri dhidi ya Jamhuri ya Ireland, kupitia mabao ya Sami Khedira, Andre Schuerrle na Mesut Özil, ili kujihakikishia nafasi ya kwanza katika kundi C, na kufika katika tamasha hilo maarufu la soka kwa mara ya 16 mfululizo.

Marouane Fellaini wa Ubelgiji (Kulia) akipambana na Mcroatia Ivan Strinic (Kushoto) na Mateo Kovacic (Katikati)
Marouane Fellaini wa Ubelgiji (Kulia) akipambana na Mcroatia Ivan Strinic (Kushoto) na Mateo Kovacic (Katikati)Picha: Reuters

Kwa Ubelgiji, hata hivyo, itakuwa mara yao ya kwanza katika Kombe la Dunia baada ya 12 baada ya kile kinachofahamika kama kizazi kipya cha nchi hiyo kuongoza kundi A kwa ushindi wa mabao mawili kwa moja dhidi ya Croatia, huku Romelu Lukaku akitikisa wavu mara mbili. Uswisi iliipiku Albania mabao mawili kwa moja na kuongoza kundi E na kujihakikishia nafasi nchini Brazil wakati kumesalia mechi moja. Uhispania ilitoka jasho na kuibwaga Belarus magoli mawili kwa moja kupitia Xavi Hernandez na Alvaro Negredo katika kipindi cha pili, na sasa inahitaji tu pointi moja kutokana na mchuano ujao wa nyumbani itakapocheza na Georgia ili kujihakikishia nafasi ya kulitetea kombe hilo mwaka ujao.

England iliendelea kuongoza kundi H, ikiwa na pengo la pointi moja mbele ya Ukraine, baada ya kuonyesha mchezo mzuri katika kipindi cha pili ambapo iliishinda Montenegro mabao manne kwa moja, huku washambuliaji Wayne Rooney na Daniel Sturridge pamoja na Andros Townsend ambaye alipewa fursa ya kuichezea timu ya taifa kwa mara ya kwanza, wakiwa wafungaji.

Wabelgiji wamesheherekea usiku kucha kufuatia kufuzu timu yao ya taifa katika dimba la dunia
Wabelgiji wamesheherekea usiku kucha kufuatia kufuzu timu yao ya taifa katika dimba la duniaPicha: Reuters

Vijana hao wa kocha Roy Hodgson wanahitaji tu ushindi dhidi ya Poland Jumanne wiki ijayo na kufuzu moja kwa moja, lakini wakitoka sare, watawapa nafasi Ukraine ambao waliwabwaga Poland bao moja kwa nunge, na wana mchuano rahisi uliosalia dhidi ya San Marino. Urusi waliwazaba Luxembourg mabao manne kwa sifuri na sasa wako mbele ya Ureno kwa tofauti ya pointi tatu huku wakihitaji tu sare dhidi ya Azerbaijan ili kujihakikishia nafasi ya kwanza. Ureno ilifungwa goli zikisalia dakika tano mchezo kuisha na ikatoka sare goli moja kwa moja na Israel. Ugiriki iliipiku Slovakia bao moja kwa sifuri na wako pointi moja na Bosnia ijapokuwa na hasara ? ya magoli. Kwingineko, Sweden ilijiunga na Croatia katika mechi za mchujo, baada ya kumaliza wa pili nyuma ya Ujerumani kwa kuwashinda Austria magoli mawili kwa moja huku Zlatan Ibrahimovic akifunga bao la ushindi.

Italia ambayo ilifuzu pamoja na Uholanzi mwezi uliopita, ilitoka sare ya mabao mawili kwa mawili na Denmark na kuwaacha Bulgaria katika nafasi ya pili kwa tofauti ya mabao katika kundi B, licha ya kichapo cha mabao mawili kwa moja na Armenia. Iceland ilisalia nyuma ya Uswisi baada ya kuizidi nguvu Cyprus mabao mawili mtungi, wakati Uturuki na Romania zikishinda mechi zao matokeo yaliyowapa pointi sawa nyuma ya Uholanzi huku kukiwa na mchuano mmoja uliosalia. Kwa ujumla, 13 kati ya nafasi 32 ZA Kombe la Dunia sasa zimejulikana. Marekani, Argentina, Australia, Costa Rica, Iran, Japan na Korea Kusini zilikuwa tayari zimejikatia tikiti, wakati Brazil ikipata kibali cha moja kwa moja kama mwenyeji wa dimba hilo.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP

Mhariri: Josephat Charo