Ujerumani: Seehofer asema hana shida tena na Merkel
8 Julai 2018Kulingana na mazungumzo aliyoyafanya na gazeti la Bild am Sonntag la hapa Ujerumani, Horst Seehofer amesema viongozi wa vyama vinavyounda serikali ya Ujerumani, hivi sasa wanatazama mbele, wakiziacha nyuma tofauti kuhus sera ya wahamiaji iliyotishia kuisambaratisha serikali hiyo.
Amesema viongozi hao walikubaliana kuwakataa wahamiaji ambao wameshaomba hifadhi katika nchi nyingine za Ulaya, kupitia mikataba na nchi nyingine ambayo bado haijasainiwa.
Seehofer aliyetaka hatua thabiti zaidi, ameliambia Bild am Sonntag kuwa makubaliano hayo yanawasilisha ishara kwa ulimwengu mzima kuwa uhamiaji haramu haufai.
Yaliyopita si ndwele
Alipoulizwa juu ya uhusiano wake na Angela Merkel amesema, yaliyopita si ndwele, na kwamba muhimu ni yaliyoko mbele.
Seehofer ambaye ni mkuu wa chama cha Christian Social Union (CSU) cha jimboni Bavaria, ambacho ni mshirika mkuu wa chama cha Christian Democratic Union (CDU) cha Kansela Merkel, amesema serikali iko njiani kuondoa kero zinazokipa umaarufu chama cha AfD, ambacho uchunguzi wa maoni wa hivi karibuni imeonyesha kwamba kinazidi kujiongezea wafuasi.
Wiki iliyopita msimamo mkali wa Horst Seehofer ulitishia kuisambaratisha serikali ya mseto wa vyama inayoongozwa na Kansela Merkel, hususan baada ya kutishia kujiuzulu ikiwa matakwa yake ya kuwafukuza mpakani wahamiaji waliosajiliwa katika nchi nyingine, yangeendelea kupuuzwa na Kansela Merkel.
Wiki hii vyama vitatu vinavounda serikali hiyo vilipata makubaliano ya kuharakisha mchakato wa kuwafukuza wahamiaji waingiao Ujerumani kutoka nchi nyingine za Ulaya, kwa kuheshimu sheria zilizopo katika Umoja wa Ulaya.
Mwandishi: Daniel Gakuba/dpae, ape
Mhariri: John Juma