Ujerumani na Uturuki zaazimia kurejesha uhusiano wa kawaida
8 Machi 2017Katika maelezo yake kwa vyombo vya habari baada ya mkutano na mwenzake wa Uturuki mjini Berlin Jumatano asubuhi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Sigmar Gabriel amesema hakuna njia mbadala kwa mazungumzo katika kuboresha hatua kwa hatua, uhusiano kati ya Ujerumani na Uturuki, licha ya tofauti na malumbano vilivyojitokea baina ya nchi hizo hivi karibuni.
Hata hivyo, Gabriel amesema kuna mstari usioweza kuvukwa, zikiwemo kauli za viongozi wa Uturuki kuilinganisha serikali ya sasa ya Ujerumani na utawala wa wanazi.
Mvutano wa sasa umeckolezwa na uamuzi wa miji kadhaa ya Ujerumani kufuta mikutano ya hadhara iliyokuwa imepangwa na mawaziri wa Uturuki, kupigia debe kura ya ndio katika kura ya maoni itakayofanyika mwezi kesho, kuhusu mabadiliko ya katiba ambayo yananuia kumpa madaraka makubwa Rais Recep Tayyi Erdogan.
Cavusoglu asema Ujerumani ina uhasama wa kimfumo dhidi ya Uturuki
Akizungumza katika ubalozi mdogo wa Uturuki katika mji wa Hamburg Kaskazini mwa Ujerumani hapo jana, waziri Cavusoglu alisema kufutwa kwa mikutano ya mawaziri wenzake haikuwa kazi ya serikali za majimbo kama inavyoelezwa na Ujerumani.
''Tafadhali msiseme ni uamuzi wa serikali za mikoa. Kuliko na shinikizo la polisi na vyombo vya upelelezi, sio kazi ya serikali za majimbo, ni mfumo.'' amedai Cavusoglu.
Cavusoglu aliitoa hotuba yake katika baraza la Ubalozi mdogo, kwa sababu hiyo hiyo ya kufutwa mikutano ya hadhara za mawaziri wa Uturuki. Waziri huyo aliitaka Ujerumani kuacha kuhubiri haki za binadamu na demokrasia kwa Uturuki, na kuinyoshea kidole Ulaya nzima kwa matatizo yaliyopo kuhusu dini za walio wachache, na uhalifu dhidi ya ubinadamu.
Gabriel ayatetea majimbo
Kwa upande wake, Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Sigmar Gabriel, akizungumza katika kipindi cha televisheni cha Heute Journal, alitetea uamuzi wa serikali za majimbo.
Amesema, ''Fikiria kama lingetokea jambo katika mikutano kama hiyo. Ingekuwa tatizo kubwa. Ni lazima kuunga mkono mamlaka ya majimbo ya Ujerumani, hta kama Uturuki haiamini hivyo. Walifanya kazi nzuri, ambayo ni majukumu yao.''
Juhudi za Mevlut Cavusoglu na mawaziri wenzake nchini Ujerumani, zinalenga kuwashawishi waturuki milioni 1.4 waishio Ujerumani wakiwa na haki ya kupiga kura nchini mwao.
Kiini kingine cha mvutano kati ya nchi mbili, ni kukamatwa nchini Uturuki kwa mwandishi raia wa Ujerumani mwenye asili ya Uturuki Deniz Yücel, ambaye serikali ya Uturuki inamtuhumu kuwa jasusi.
Sigmar Gabriel alikuwa amesema angefanya lolote awezalo kuhakikisha mwandishi huyo anaachiwa huru, akisema watu kama yeye wanaweza kuwa daraja linaloziunganisha nchi mbili.
Mwandishi: Daniel Gakuba/rtre, afpe, dpae
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman