Ujerumani na Ureno zaingia robo fainali UEFA EURO 2012
18 Juni 2012Lukas Podolski alicheza mchezo wake wa 100 katika kikosi cha Ujerumani na kufunga bao katika dakika ya 19 kabla ya Michael Krohn-Dehli kusawazisha kwa upande wa Denmark dakika tano baadaye lakini beki Lars Bender akatikisa wavu na kuwahakikishia Ujerumani nafasi ya kupambana na Ugiriki katika robo fainali.
Nayo Ureno iliiondoa Uholanzi mbele ya maelfu ya mashabiki wao waliovalia jezi za njano na kuwashangilia kana kwamba walikuwa katika uwanja wa nyumbani. Ronaldo alisawazisha bao lake Rafael van der Vaart katika dakika ya 28, na kisha mchezaji huyo anayelipwa fedha nyingi zaidi ulimwenguni akamaliza kazi kwa kufunga bao la ushindi zikiwa zimesalia dakika 16 mchezo kukamilika.
Ujerumani sasa watapambana na Ugiriki ambao walisababisha mshangao mkubwa katika kinyang'anyiro hicho wakati walipowazaba Urusi goli moja kwa sifuri na kuwafurusha vijana hao wa kocha Dick Advocat.
Torres awaonya wenzake
Mshambuliaji wa Uhispania Fernando Torres amewaonya wenzake kujifunza kutokana na kuondoka mapema kwa Urusi na kutozembea wakati watakapoingia uwanjani leo dhidi ya Croatia. Torres anatumai kuwa Uhispania watakuwa macho wakati kipenga cha kuanza mechi kitakapopulizwa na akawataka wenzake wakumbuke kilichowatokoea Warusi walioanza mechi zao kwa ushindi, lakini wakatolewa kwa kufungwa goli moja kwa sifuri na Ugiriki.
Uhispania wako pointi nne sawa na Croatia katika kundi C, huku sare ikitosha kuwapeleka katika robo fainali.
Mabingwa hao wa kombe la dunia watatolewa tu ikiwa watashindwa mchuano huo, na kisha Italia iichape Ireland ambayo tayari imeondolewa.
Uhispania na Croatia wanaweza kufuzu ikiwa watatoka sare ya magoli mawili kwa mawili. Katika mchuano wa pili, Italia itakutana na Jamhuri ya Ireland. Italia ni lazima washinde na watalazimika kucheza bila huruma yoyote na kuomba msaada kutoka kwa mchuano wa Uhispania na Croatia.
Katika mechi za Jumanne,
Kwa maelfu ya mashabiki wa Ukraine, hatima ya timu yao ya soka itajulikana usiku mjini Donesk. Ni ushindi pekee dhidi ya Uengereza ndio utakaoiweka Ukraine katika dimba hilo ambalo nchi hiyo ilifanya bidii kuliandaa.
Wakati Wayne Rooney akitarajiwa kurejea baada ya kukosa mechi mbili za kwanza, WaUkraine huenda wasiwe na mshambulaji wao Andriy Shevchenko ambaye ana jeraha la goti. Mshambuliaji huyo wa klabu ya Dynamo Kiev ndiye aliyefunga magoli ya pekee ya nchi yake katika kinyang'anyiro hicho. Sare itatosha kuwapa tiketi Uingereza na wakishindwa basi wataomba Ufaransa ishindwe na Sweden.
Ufaransa ni lazima iizabe Sweden ambayo haina cha kunufaika kutokana na mchuano wao wa mwisho katika tamasha hilo. Mchuano huo unaweza kuonyesha mwamko mpya kwa Ufaransa ambayo haijawahi kufika katika robo fainali ya dimba lolote tangu kombe la dunia la mwaka wa 2006.
Ikiwa Ufaransa itafanikiwa kumaliza ya kwanza katika kundi D itaepuka kukutana na mabingwa Uhispania katika timu nane za mwisho, mradi tu Uhispania imalize mbele ya mahasimu wao Croatia na Italia katika kundi C.
Mwandishi: Bruce Amani/Reuters/AP/AFP
Mhariri:Miraji Othman