Ujerumani na juhudi za kuleta amani Kima
7 Desemba 2015.Rais Joachim Gauck yuko Jordan alikowasili akitokea Israel na Palestina ambako amezitolea mwito pande zote mbili kutoa nafasi ya pili kwa mazungumzo ya kusaka amani katika eneo hilo.
Tukianzia na ziara ya rais Joachim Gauck mashariki ya kati ambapo leo amezungumza na mfalme Abdullah wa Jordan amebaini kwamba Ujerumani inaunga mkono mapambano ya kukabiliana na kundi la wanamgambo wa itikadi kali linalovuruga usalama katika nchi za Syria na Iraq pamoja na kuwasaidia wakimbizi wanaotoroka mgogoro katika nchi ya Syria.
Aidha rais huyo wa Ujerumani ameisifu Jordan kwa kuwa mshirika mkubwa anayesaidia katika kulishughulikia wimbi la wakimbizi kutoka Syria.
Jumapili rais huyo wa Ujerumani alipokuwa ziarani Jerusalem aliwatolea mwito viongozi wa Palestina na Israel kuweka pembeni mivutano na kukaa tena katika meza ya majadiliano kutofuta makubaliano ya amani.
Steinmeier Iraq
Ama kwa upande mwingine Juhudi za kutuliza migogoro zinafanywa pia na waziri wa mambo ya nje Frank Waltersteinmeier aliyeko Iraq ambako hii leo amekutana na waziri mkuu Haider al Abadi ambaye ameitaka Ujerumani kutoa msaada zaidi katika mapambano na kundi la dola la kiislamu nchini Iraq.
Iraq imeitaka serikali ya Ujerumani kusaidia katika kutoa mafunzo kwa vikosi vyake katika wakati ambapo wanajeshi wa Ujerumani wanatoa mafunzo kwa wanajeshi wakikurdi tu kaskazini mwa Iraq.Aidha waziri Steinmeir kwa upande wake ametumia nafasi ya ziara hii kuzungumzia hatua ya hivi karibuni ya jeshi la Iraq kufanikiwa kuidhibiti tena miji kadhaa ya Iraq ambayo awali ilidhibitiwa na dola la Kiislamu.Ziara ya Steinmeier ni ya ghafla nchini Iraq iliyoanza hapo jana.
Von Der Leyen Afghanistan
Halikadhalika waziri wa ulinzi Ursula von Der Leyen naye yupo nchini Afghanistan tangu jana ambako aliwatembelea wanajeshi wa Ujerumani huko Kaskazini mwa nchi hiyo ikiwa ni ziara inayofanyika baada ya serikali ya Ujerumani hivi karibuni kutoa uamuzi wa kutanua hatua za kupeleka wanajeshi wake nchini humo.Katika ujumbe wake nchini humo Von Der Leyen amewaambia waafghanistan kwamba wanajeshi wa Ujerumani wataendelea kubakia Afghanistan.Wanajeshi wa Ujerumani wako Mazar-I-Sharif ambako wanajeshi 1500 kutoka nchi 21 za Jumuiya ya Nato wamepiga kambi wengi wakiwa ni kutoka Ujerumani.Ujerumani inapanga kuongeza wanajeshi wake huko kutoka 850 hadi 980.
Mwandishi Saumu Mwasimba
Mhariri:Abdul-Rahman